Picha Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
TAARIFA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU
YA KIMATAIFA YA MTOTO WA KIKE ITAKAYOFANYIKA TAREHE 11 OKTOBA, 2017
KATIKA WILAYA YA TARIME, MKAONI MARA
Ndugu Wanahabari,
Awali ya yote, napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha sote
kukutana mahali hapa. Pili, napenda kuwashukuru waandishi wa habari wote
mliohudhuria kikao hiki, kwani kupitia kwenu Serikali itapata fursa ya
kupeleka ujumbe maalum kwa wazazi, walezi na Watanzania wote kuhusu
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike kwa mwaka 2017.
Tarehe 11 Oktoba ya kila mwaka
Tanzania inaungana na Nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika
kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. Kwa mwaka huu,
Maadhimisho hayo yatafanyika wilaya ya Tarime mkoani Mara. Mkoa wa Mara
ni miongoni mwa mikoa 5 inaoongoza kwa mimba za utotoni ambayo ni Katavi
(45%), Tabora (43%), Dodoma (39%), Mara (37%) na Shinyanga (34%).
Ndugu Wanahabari,
Katika kufanikisha maadhimisho ya
mwaka, wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imepanga kufanya
shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya kujitambua na afya ya uzazi
ili watoto wa kike waweze kujilinda na mimba za utotoni. Aidha,
uhamasishaji utafanyika kwa lengo la kujenga uelewa kwa waendesha
Bodaboda kuhusu madhara ya mimba za utotoni na kujali utu wa mtoto wa
kike. Vilevile kutafanyika Kongamano la watoto ambalo litawapa watoto
nafasi kujadili changamoto zinazowakabili ikiwemo masuala ya ukatili.
Sambamba na hili kutakuwa na Kongamano la Wazazi, walezi, viongozi wa
dini na watu mashuhuri watakaojadili changamoto za malezi kwa mtoto.
Ndugu Wanahabari,
Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘’Tokomeza Mimba za Utotoni; Tufikie Uchumi wa Viwanda’’
Kaulimbiu hii inasisitiza kupiga vita kwa nguvu zote mila na desturi
zenye athari kwa watoto zenye kupelekea mimba za utotoni na kuathiri
maendeleo ya mtoto wa kike na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi. Kuna
usemi kuwa kumwendeleza mtoto wa kike ni kuendeleza familia na taifa kwa
kuwa mchango wa mwanamke katika uchumi wa nchi ni mkubwa kwa kuzingatia
idadi ya wanawake ukilinganisha na wanaume hapa nchini. Kundi hili lina
mchango mkubwa katika ujenzi na maendeleo ya viwanda nchini. Hivyo
tabia na mienendo yote yenye viashiria vya kusababisha mimba kwa watoto
wa kike ni lazima vidhibitiwe. Hii itasaidia kuwa na watoto
watakaowezesha taifa kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka
2030.
Ndugu Wanahabari,
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani
(WHO) ya mwaka 2014 inaonyesha kuwa asilimia 11 ya wanawake
waliojifungua walikuwa na umri kati ya miaka 15 -19.
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Utoto
na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2015 unaonyesha kuwa asilimia
27% ya watoto wa kike wanapata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18.
Aidha, taarifa ya utafiti ya hali ya ukatili dhidi ya watoto
iliyotolewa mwaka 2011 unaonyesha kuwa kwa kila watoto wa kike 3 mtoto
1 (27.9%) amefanyiwa vitendo vya ukatili na takribani asilimia 6.9
walilazimishwa kufanyiwa ukatili wa kingono.
Ndugu Wanahabari,
Katika kukabiliana na changamoto
mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike Serikali kwa kushirikiana na
wadau imeanza kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili
dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 -2021/22). Mpango huu umelenga
kupunguza ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/22
na tunatarajia kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 hadi
kufikia asilimia 5.
Mwisho
Ndugu Wanahabari,
Ni matarajio yangu kuwa wanahabari
mtaendelea kuhamasisha umma kuhusu kaulimbiu na kuhamasisha wananchi
kujitokeza katika Maadhimisho ya siku hii ili kuimarisha utoaji haki
sawa kwa watoto wote ikiwa ni pamoja na kutokomeza mimba za utotoni kwa
watoto wa kike walioko masomoni ili kutimiza ndoto zao.
Nawashukuru sana kwa kukubali mwaliko wa wizara kuja kuwa nasi kwa siku ya leo.
Asanteni kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment