Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Wataalamu wa majadiliano ya
mikataba wametakiwa kuweka maslahi ya Taifa mbele wanapoandaa mikataba
ya kimataifa ili kulinda na kusimamia raslimali za nchi.
Wito huo umetolewa jana na Naibu
Mwansheria Mkuu wa Serikali, Gerson Mdemu wakati akifunga mafunzo ya
maafisa waandamizi wa serikali za nchi tisa za kiafrika kuhusu
majadaliano ya mikataba ya kibiashara ya kimataifa yaliyofanyika jijini
Dar es Salaam.
Mdemu aliwasititiza washiriki wa
mafunzo hayo kutumia ujuzi walioupata kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika
kwa majuma mawili kwa ajili ya maslahi ya nchi zao ili kulinda raslimali
za nchi husika ili zitumike kwa manufaa ya umma.
“Tangulizeni maslahi ya nchi na si
ya kwenu binafsi katika mikataba ya kimataifa na kuondokana na vitendo
vya rushwa”, alisema Mdemu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Mafunzo wa Uongozi Institute, Kadari Singo amesema mafunzo hayo
yameandaliwa kutokana na nchi za kiafrika kuwa nyuma katika majadaliano
ya mikataba ya kimataifa.
“Tumeamua kufanya mafunzo haya
kuwafundisha maafisa waandamizi toka nchi za kiafrika ili kuwapa ujuzi
na utaalamu wa kufanya majadiliano ya mikataba ili iweze kuwa na manufaa
kwa nchi husika”, alisema Singo.
Kwa mujibu wa Bwana Singo, mafunzo
ya aina hiyo yatakuwa endelevu kwa watumishi wa Serikali ii kuiwajengea
uwezo katika eneo hilo na yatakuwa yakifanyika kujumuisha wataalam wa
sekta husika kama vile, sekta madini, misitu, wanyamapori na sheria.
Aidha, Singo alisema mafunzo haya
yatahakikisha yanapinga vikali vitendo vya rushwa kwenye mikataba ili
kuzinusuru nchi za kiafrika kutumbukia katika mikataba isiyowanufaisha
wananchi.
Mafunzo haya yameandaliwa na
Uongozi Institute na yamewajumuisha watumishi wa serikali waandamizi
kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Kenya, Ghana, Nigeria, Uganda, Namibia
na wenyeji Tanzania.
Hivi karibuni, Mheshimiwa Rais
John Pombe Magufuli wakati akipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa
mchanga wa madini alimtaka Spika wa Bunge kutumia Bunge lake kupitia
sheria za madini ili kuhakikisha sheria hizo zinaleta manufaa kwa
wananchi.
Mikataba ya madini na mali za asli
nyingine imekuwa ikipigiwa kelele kuwa haina lengo la kuinufaisha nchi
bali watu wa nchi nyingine. Hivyo Miswada ya Maliasili za nchi
imepelekwa Bungeni kwa Hati ya Dharula ili kutoa nafasi ya kutunga
sheria mapema iwezekanavyo za kuleta manufaa na tija kwa nchi hasa
kupitia madini na maliasili nyingine zikiwemo mbuga za wanyama na
hifadhi nyingine za Taifa.
Kwa kuzingatia unyeti na umuhimu
wa suala hilo, muda wa kumaliza Bunge umeongezwa badala ya kumaliza Juni
30 sasa litaenda hadi Julai 5, 2017.
No comments:
Post a Comment