Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Ephraim Kwesigabo (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa
mwezi Juni, 2017 ambao umepungua hadi asilimia 5.4 kutoka asilimia 6.1
mwezi Mei, 2017. Kushoto kwake ni Meneja wa Takwimu za Bei na Ajira,
Ruth Minja.
Baadhi
ya Waandishi wa habari waliohudhuria katika Mkutano wa kutangaza
Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Juni, 2017 uliofanyika leo jijini Dar
es Salaam. Mfumuko wa bei umeonyesha kupungua hadi asilimia 5.4 kutoka
asilimia 6.1 mwezi Mei, 2017. ( PICHA NA EMMANUEL GHULA)
Na: Veronica Kazimoto, Dar es Salaam,
Mfumuko
wa Bei wa Taifa kwa mwezi Juni, 2017 umepungua hadi asilimia 5.4
ikilinganishwa na asilimia 6.1 ilivyokuwa mwezi Mei, 2017.
Akizungumza
na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa ya
Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim
Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei umepungua kutokana na kupungua kwa kasi
ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Juni, 2017
ikilinganishwa na kasi ya upandaji iliyokuwa kwa mwezi Mei, 2017.
“Mfumuko
wa Bei wa mwezi Juni, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka
asilimia 6.1 mwezi Mei, 2017. Hii inatokana na kupungua kwa kasi ya
upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Juni, 2017,” amesema
Kwesigabo.
Amesema
Mfumuko wa Bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umepungua kwa asilimia
0.1 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.2 ilivyokuwa mwezi Mei,
2017.
Kwesigabo
amesema Fahirisi za Bei zimepungua hadi 109.10 mwezi Juni, 2017 kutoka
109.26 mwezi Mei, 2017. Amesema Kupungua kwa Fahirisi za Bei
kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.
Baadhi
ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa fahirisi ni pamoja na
mahindi ambayo yamepungua kwa asilimia 5.1, unga wa mahindi kwa asilimia
2.4, unga wa mihongo kwa asilimia 1.9, machungwa kwa asilimia 2.4,
dagaa kwa asilimia 3.2, mbogamboga kwa asilimia 5.7, maharage kwa
asilimia 1.8 na viazi mviringo kwa asilimia 6.2.
Aidha
Mfumuko wa Bei kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi
Juni, 2017 umepungua hadi asilimia 9.8 kutoka asilimia 11.8 mwezi Mei,
2017.
Uwezo
wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeimarika
kidogo na kufikia Shilingi 91 na senti 66 mwezi Juni, 2017
ikilinganishwa na Shilingi 91 na senti 53 ilivyokuwa mwezi Mei, 2017.
Hata
hivyo, Mfumuko wa Bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi
ya nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi
Juni, 2017 nchini Uganda umepungua hadi asilimia 6.4 kutoka asilimia 7.2
mwezi Mei, 2017; na nchini Kenya, Mfumuko wa Bei wa Mwezi Juni, 2017
umepungua hadi asilimia 9.21 kutoka asilimia 11.70 mwezi Mei, 2017.
No comments:
Post a Comment