Na Christina Mwangosi, MOHA
Kamishna Jenerali wa Jeshi la
Magereza nchini Dk. Juma Malewa amesema Jeshi la Magereza nchini litatoa
elimu ya namna kila Mtanzania hata aishie kwenye nyumba za ghorofa ama
maeneo yenye nafasi ndogo ya kuanzisha kilimo cha mbogamboga, anavyoweza
kutumia eneo dogo kuendeshea shughuli za kilimo cha mbogamboga wakati
huu Maonyesho ya SabaSaba yanayoendelea katika Viwanja vya SabaSaba
jijini Dar es salaam.
Kamishna Jenerali Dk. Malewa
amesema kuwa pamoja na kuandaa Shamba Darasa kwa ajili ya kutoa elimu ya
shughuli mbalimbali za kilimo, Jeshi la Magereza limeandaa bidhaa
mbalimbali ambazo zitaonyeshwa wakati wote wa Maonyesho pamoja na kuuzwa
wakati wote wa Maonyesho hayo.
Dk. Malewa amesema miongoni mwa
bidhaa hizo ambazo ziko kwenye Banda la Magereza ni samani mbalimbali
kwa ajili ya matumizi ya ofisi na nyumbani ikiwemo makabati ya vyombo na
nguo, meza na viti, madawati kwa ajili ya shule za msingi na
sekondari, vitanda, sofa, ‘dressing table’ pamoja na viatu vya ngozi
vya kike na kiume.
Amesema Jeshi la Magereza pia
litauza pia majiko sanifu yanayotumia kuni kidogo, mashuka, foronya,
vikoi pamoja na sabuni zenye ubora kwa ajili ya kufua nguo ambazo
zinatengenezwa katika Kiwanda cha Sabuni kilichopo Mkoa wa Mbeya.
Amesema Jeshi la Magereza katika
kipindi hiki cha Maonyesho litatoa elimu ya shughuli za kilimo cha
kisasa bure na kwa wale wananchi ambao maeneo yao yanafikika Wataalamu
wa Magereza wanaweza kuwatembelea wananchi kwenye maeneo yao na
kuwafundisha namna ya kuanzisha kilimo hicho kinachojulikana kama
‘kilimo cha jikoni’.
No comments:
Post a Comment