Wednesday, 5 July 2017

Dkt. Tulia Ackson ajirudi kwa kauli zake

  PIX 1 Mhe.Tulia
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson.
Naibu spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt.  Tulia Ackson  amefunguka na kusema wabunge wa upinzani muda mwingine huwa wanaleta hoja nzuri kwa serikali lakini serikali inashindwa kuzipokea hoja hizo kutokana na uwasilishaji wao.
Naibu Spika amesema hayo leo Dodoma wakati akifanyiwa mahojiano katika kipindi cha bunge, ambapo alikuwa akitoa mtazamo wake juu ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka 2017/2018
"Wabunge wa upinzani muda mwingine wanaleta hoja nzuri sana bungeni lakini tatizo kubwa linakuja katika lugha inayotumika inakuwa si lugha ya staha ndiyo maana unaona hata serikali inakuwa haikubali. Bunge ni jumba la kisiasa, hivyo kila mwamba ngoma huvutia kwake, upande wa chama kinachoongoza ndiyo chenye serikali wana namna yao ya kuishauri serikali, ila wale ambao wanataka kuingia madarakani nao wana namna yao ya uchangiaji bungeni ndiyo maana kuna kuwa na mvutano wa hapa na pale" alisema  Tulia Ackson
Mbali na hilo Naibu Spika alidai serikali muda mwingine imekuwa inashindwa kufanyia kazi kwa haraka baadhi ya ushauri wa wabunge utolewao bungeni kutokana na ukweli kwamba serikali kabla ya kuleta jambo bungeni huwa inakuwa imefanya utafiti wa kutosha, hivyo linapoibuka jambo jipya inakuwa changamoto, inabidi ilichukue na kuja kulifanyia kazi siku za mbeleni.


Kuhusu upendeleo bungeni Naibu Spika amesema wabunge wote wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wapinzani wamekuwa wakipewa nafasi sawa lakini wabunge wa upinzani wamekuwa wakilalamika kutokana na kuwa na dhana ya kuonewa.

"Bunge hili limekuwa na wabunge zaidi ya 300 na walio wengi zaidi ni wabunge kutoka chama tawala, hivyo wale wa upinzani kwa kuwa wapo wachache hivyo wanaweza kuona kama wanaonewa hivi, wanaweza kuona kama hawasikilizwi, wanaona kama hawapewi muda zaidi, lakini unakuta mtu ukiwa kwenye kile kiti unawaza hili na kufanya utende kwa usawa tena kwa kuwasaidia walio wachache ili dhana hiyo isiwepo" alisisitiza Tulia Ackson

Kwa kumalizia  Tulia Ackson  aligusia jambo la mbunge kulishtaki bunge mahakamani na kusema kuwa hakuna mbunge anaweza kulishtaki bunge kama taasisi

"Bunge kama taasisi likifanya jambo huwezi kulipeleka mahakamani, bunge likiwa limefanya maamuzi juu ya jambo fulani na ukaona bunge halijafanya sawa kuna utaratibu wa kibunge lakini huwezi kuchukua maamuzi ya bunge ukapeleka mahakamani, kwa hiyo kuna utaratibu wake, lakini uamuzi wa bunge huwezi kuupeleka mahakamani kikanuni" alimalizia  Tulia Ackson

No comments:

Post a Comment