Wakati kesho Jumatano Julai 5,
2017 timu yetu ya Tanzania ya mpira wa miguu – Taifa Stars ikicheza na
Zambia katika Nusu Fainali ya kuwania Kombe la Castle COSAFA, Kocha Mkuu
Salum Shaban Mayanga amemuongeza kwenye kikosi Mshambuliaji John
Raphael Bocco.
Bocco kwa sasa yuko Afrika Kusini
pamoja na timu hiyo akichukua nafasi ya Mshambuliaji Mbaraka Yussuf
Abeid aliyejepata majeruhi kwenye michuano hiyo iliyoanza Juni 25, mwaka
huu ambako Tanzania ilikuwa Kundi ‘A’ pamoja na timu za Malawi,
Mauritius na Angola.
Tanzania iliibuka kinara katika
kundi hilo na kucheza Robo Fainali ambako ilicheza na Afrika Kusini na
kuitoa katika hatua hiyo hivyo kwa mujibu wa ratiba, kesho Jumatano
Julai 5, mwaka itashindana na Zambia.
Kocha Salum Mayanga amefafanua
kuwa mbali ya Bocco kujaza nafasi hiyo, amemwongeza kwenye kikosi ili
kuongeza nguvu ya kupambana na Rwanda katika mchezo wa kufuzu fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani –
CHAN.
Mchezo dhidi ya Rwanda utafanyika
Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Mchezo
wa marudiano utafanyika baadaye mwezi huu au mapema mwezi ujao na
mshindi wa jumla atacheza na Uganda. Mshindi wa jumla kati ya Tanzania
na Uganda ndiye atakayefuzu kwa fainali za CHAN zitakazofanyika Kenya,
mwaka 2018.
No comments:
Post a Comment