Na Daudi Manongi,MAELEZO,DODOMA.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa
ameelekeza Baraza la Michezo Tanzania(BMT) livunjwe na shughuli zake
kufanywa na Sekretarieti hadi hapo Baraza jipya litakapoundwa tena.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo
leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akisoma hotuba ya kuhairisha mkutano wa
saba wa Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Serikali ya awamu ya tano
haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali
maslahi ya Taifa,Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya
michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo”,Aliongeza
Mhe.Majaliwa.
Aidha katika hotuba yake
amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk John Pombe
Magufuli kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya
kujenga Uwanja mkubwa wa Michezo hapa mjini Dodoma kwa kushawishi
mataifa rafiki kama vile Moroco ambao wanajenga uwanja huo.
Pia amesema kuwa Serikali
inatambua umuhimu wa michezo kwa Afya,umoja wa kitaifa na kama fursa ya
ajira kwa vijana wetu ambapo ivi karibuni mkoani Mwanza yamehitimishwa
mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yaliyoibua vipaji na hamasa
kubwa iliyo miongoni mwa vijana nchini.
“Tutaendelea kuratibu michezo
shuleni,ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa michezo kama
somo,maelekezo yetu ni kwamba kila mkoa uwe na shule angalau mbili zenye
mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha
michezo,Ameeleza Mhe.Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa pia
ameipongeza kwa dhati timu ya Serengeti Boys kwa kutoa upinzani mkubwa
kwenye mashindano ya shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika na
kuweka msisitizo kwa Chama cha Mpira nchini(TFF) kuendelea kuwatunza
vijana hao.
“Msisitizo wangu kwa TFF ni
kuendelea kuwatunza vijana hao na kusimamia vilabu vya michezo nchini,
kuwekeza kwenye soka la vijana ili kujenga timu imara kwa miaka michache
ijayo”,Aliongeza Mhe.Majaliwa.
No comments:
Post a Comment