Rais wa Marekani Trump amethibitisha kwamba anachunguzwa yeye binafsi
kutokana na hatua yake ya kumfuta kazi mkuu wa Shirika la Uchunguzi wa
Jinai la Marekani FBI James Comey.
Kupitia Twitter, Bw Trump amekariri kwamba uchunguzi unaoongozwa na
mwendesha mashtaka maalum kuhusu tuhuma kwamba maafisa wa Urusi
waliingilia uchaguzi wa mwaka 2016 ili kumfaa Trump hauna msingi.
Ni mara ya kwanza kwa Bw Trump kuzungumzia taarifa kwenye magazeti
kwamba anachunguzwa kwa tuhuma za kuhujumu mifumo ya haki kwa kumfuta
kazi Bw Comey.
Awali, taarifa kwenye vyombo vya habari Marekani vilikuwa vimeripoti
kwamba wasaidizi wake pamoja na watu waliojitolea kusaidia katika kundi
lake la mpito wameamrishwa kuhifadhi nyaraka zote kuhusiana na uchunguzi
huo wa madai kuhusu Urusi.
Taarifa zinasema mawakili wa maafisa hao wa Trump wametakiwa kuhifadhi
nyaraka zote zinazohusiana na Urusi, Ukraine na washauri wengine kadha
wa kampeni.
Kuna makundi kadha yanayofanya uchunguzi, kundi moja likiongozwa na
mkurugenzi wa zamani wa FBI Robert Mueller, ambayo yanachunguza iwapo
maafisa wa Trump walishirikiana na maafisa wa Urusi wakati wa kampeni.
No comments:
Post a Comment