Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati)
akisaini Mkataba kwa niaba ya Serikali na Klabu ya Yanga ya jijini Dar
es salaam ambayo iliwakilishwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu hiyo Baraka
Deusdedit (kulia) leo jijini Dar es salaam. Mkataba huo unahusu Klabu
ya Yanga kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa na Uwanja wa Uhuru katika mechi za
Kimataifa na Ligi Kuu. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Sheria Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Evordy Kyando.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akibadilishana
Mkataba waliosaini na Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga Baraka
Deusdedit leo jijini Dar es salaam. Mkataba huo unahusu Kalabu ya Yanga
kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa na Uwanja wa Uhuru, Wa kwanza kushoto ni
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Alex Nkenyenge.
Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel (wa pili kushoto) mara baada ya kusaini Mkataba na Klabu ya
Yanga leo jijini Dar es salaam. Wa pili kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa
Klabu ya Yanga Baraka Deusdedit.
YANGA KUTUMIA UWANJA WA TAIFA KWA MICHEZO YA LIGI KUU NA KIMATAIFA
Na Eleuteri Mangi – WHUSM
02 Desemba, 2016
Dar es Salaam.
Serikali imesaini Mkataba na Klabu
ya Yanga kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa pamoja na Uwanja wa Uhuru kwa
ajili ya michezo yote ya Kimataifa pamoja na michezo ya Ligi Kuu ya
ndani.
Mkataba huo umesainiwa leo jijini
Dar es salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya Serikali na Kaimu Katibu
Mkuu wa Klabu ya Yanga Baraka Deusdedit kwa niaba ya Klabu ya Yanga.
Katika Mkataba huo, Klabu ya Yanga
imeruhusiwa kutumia viwanja hivyo kama viwanja vyake vya nyumbani kwa
sharti la kuvitunza viwanja hivyo wakati wote wanapovitumia.
Miongoni mwa masharti hayo ni
kutunza viwanja, mali na vifaa vyote vilivyopo katika viwanja hivyo, na
endapo kutatokea uharibifu wowote utakaofanywa na wachezaji ama
mashabiki, Klabu hiyo itawajibika kubeba gharama za matengenezo yote
yatakayotokana na uharibifu huo.
Aidha, Klabu ya Yanga inaweza kutumia viwanja hivyo kwa mazoezi ya kujianadaa na mechi zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment