Wednesday, 21 December 2016

Polisi yatoa tamko miili 7 na kutoweka kwa Sanane

 Kaimu DCI, Kamishna Robert Boaz

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa ufafanuzi kuhusu miili 7 ya watu iliyokutwa ikielea katika mto Ruvu na kusema kuwa linaendelea na upelelezi kwa lengo la kuwatambua marehemu hao.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya JInai Kamishna wa Polisi Robert Boaz, amesema jeshi hilo bado halijawatambua marehemu hao, huku akitetea uamuzi wa jeshi hilo kuzika haraka miili ya marehemu 6 kati ya 7.
"Hatua zote za kitaalam zilifuatwa na tunaendelea kufanya upelelezi unaolenga kuwatambua marehemu hao na kujua ni jambo gani liliwasibu, tunawasihi wananchi kuendelea kutupa taarifa zitakazosaidia kutambulika kwa marehemu hao" Amesema Boaz
Akielezea jinsi jeshi hilo lilivyopata taarifa, amesema jeshi hilo lilipata taarifa za kuelea kwa maiti 7 katika mto Ruvu eneo la Mkuruge wilayani Bagamoyo kati ya tarehe 6/12/2016 hadi 9/12/2016 ambapo askari na daktari walifika katika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa kitaalam.
Amesema miili 6 kati ya 7 ilikuwa imeharibika sana na ndiyo maana iliamuliwa zizikwe katika eneo la tukio wakati moja yenye unafuu ikipelekwa hospitali ya wilaya ya Bagamoyo hadi tarehe 16/12/2016 ilipozikwa na halmashauri baada ya kutotambuliwa na tu yoyote.
Kuhusu kutoweka kwa msaidizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Ben Sanane, Kamishna Boaz amesema jeshi hilo linaendelea na upelelezi ili kubaini mahali alipo na kilichomsibu.
Hii ni sehemu ya taarifa yake.

No comments:

Post a Comment