Mkuu
wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Fabian Daqarro(mbele) akizungumza na
wananchi wa Kata ya Muriet(hawapo Pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi
wa Kituo cha Afya Muriet.
Mkurugenzi
wa Jiji la Arusha Ndg. Athumani Kihamia(mbele) akishiriki kuchimba
Msingi wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Muriet.
Wananchi
wa Kata ya Muriet wakishiriki katika Ujenzi wa Msingi wa Kituo cha
Afya, zoezi la ujenzi limezinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe.
Gabriel Daqarro.
Mkurugenzi
wa Jiji la Arusha Ndg. Athumani Kihamia akihamasisha wananchi
kuendelea kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa Kituo cha Afya Muriet
wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Kituo hicho.
Mkuu
wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Fabian Daqarro akishirkiana na
wananchi kuchimba Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Muriet.
……………………………………………………………………
Nteghenjwa Hosseah, Arusha
Wakazi zaidi ya 27,000 wa kata ya
Murriet iliyopo Jiji la Arusha wataondokana na adha ya kutembea umbali
mrefu wa zaidi ya km 15 kusaka huduma ya Afya na kujifungua kwa akina
mama baada ya Mkuu wa wilaya ya Arusha, Mhe. Gabriel Daqarro kuzindua
ujenzi wa Kituo cha Afya kitakachogharimu zaidi ya shilingi milioni 400
katika kata hiyo.
Kuanza kwa ujenzi wa Kituo cha
Afya kitakachokuwa cha kisasa ni kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya
wananchi wa eneo hilo kwa Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alipokuwa katika
ziara Mkoani Arusha hususani katika Jiji la Arusha kuwa kata hiyo yenye
wakazi hao haina zahanati wala kituo cha afya cha uhakika na kufikia
hatua ya akina mama kujifungulia nyumbani au njiani wakati wakienda
katika kituo cha Afya za Levolosi kilichopo umbali wa km 15 .
Kufuatia malalamiko hayo ya
akina mama waliokuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ya kutaka kituo
cha afya au zahanati,Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza mara moja huduma hiyo
kuwafikia wananchi bila ya kuchelewa.
Mhe. Daqarro alisema kuanza kwa
ujenzi wa kituo hicho ni kufuatia jitihada za Mkuu wa Mkoa wa
Arusha,Mhe. Mrisho Gambo kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi kama vile
matofali 3, 000, mifuko ya sementi 100 na bati 100 kwa ajili ya ujenzi
huo.
Alisema na kuwataka Halmashauri
ya Jiji kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo kufanya kila
linalowezekana kuhakikisha Kituo hicho cha Afya hiyo kinakuwa na
maabara, chumba cha Upasuaji pamoja chumba cha wagonjwa wa nje sambamba
na vifaa vya kisasa ili wananchi waliokuwa katika kata hiyo kupata
huduma na kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu.
Naye Mkurugunezi wa Jiji Ndg.
Athumani Kihamia alisema Rais Dkt. John Magufuli katika kipindi cha
kampeni aliahidi kila kata kote nchini kuwa na zahanati au kituo cha
afya cha uhakika kwa ajili ya kusongeza huduma ya afya kwa wananchi
hivyo Jiji la Arusha limeanza kutekeleza Ahadi hiyo .
Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha Dr.
Bakari Salumu alisema kuwa Jiji la Arusha linaupungufu wa vituo vya
Afya 9 na zahanati 11 kwani vilivyopo havikithi mahitaji ya wananchi kwa
sasa.
Dr. Bakari aliongeza kuwa kwa
sasa Jiji la Arusha lina zahanati 71 na vituo vya afya 16 mahitaji
ambayo bado hayakithi matwaka ya wakazi wa Jiji hilo lenye mitaa 154
ambalo linakuwa siku hadi siku.
Alisema Kituo hicho cha Afya
kinachojengwa kitakuwa na vifaa vyote muhimu na madaktari wa kutosha
kutoa huduma hiyo kwani kata hiyo ndio yenye wakazi wengi kuliko kata
yoyote katika Jiji la Arusha.
No comments:
Post a Comment