Afisa
Madini wa Geita, Fabian Mshai (aliyesimama) akitoa maelezo kwa Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati), namna
ambavyo Ofisi yake ilitekeleza maagizo aliyoyatoa kwao kuhusu malalamiko
ya baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na Mgodi wa Dhahabu wa Geita
(GGM) likiwemo suala la mipasuko ya nyumba zao. Wengine pichani ni
maafisa kutoka Wizarani.
Baadhi
ya Maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakimsikiliza Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani),
wakati alipokuwa akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Geita na wawakilishi
wa wananchi kuhusu ripoti ya wataalam wa mipasuko kutoka Wakala wa
Jiolojia Tanzania (GST) juu ya chanzo cha mipasuko ya baadhi ya nyumba
na majengo yaliyo karibu na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani akizungumza na
wawakilishi wa wananchi wa Geita wakiwamo wabunge na madiwani kuhusu
uamuzi wa Serikali kufuatia malalamiko mbalimbali yaliyotolewa na baadhi
ya wananchi wanaoishi jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kuwa
shughuli zinazoendeshwa na Mgodi huo zinawaathiri kwa namna mbalimbali.
Mbunge
wa Viti Maalum Geita (CHADEMA), Upendo Peneza, akizungumza wakati wa
kikao baina ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani na
wawakilishi wa wananchi wa Geita wakiwamo wabunge na madiwani husika
kuhusu malalamiko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wananchi wanaoishi
jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwamba shughuli zinazofanywa
na Mgodi huo zinawaathiri kwa namna mbalimbali.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati) akitoa
maagizo mbalimbali kwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kuhusu malalamiko
ya baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na Mgodi huo kuwa shughuli
zinazofanywa na Mgodi zinawaathiri kwa namna mbalimbali. Waliokaa Kulia
ni viongozi kutoka GGM. Kushoto ni baadhi ya wawakilishi wa wananchi wa
Geita wakiwamo wabunge na madiwani na Maafisa wa Wizara ya Nishati na
Madini.
Na Veronica Simba – GEITA
Serikali imetoa siku 30 kwa Mgodi
wa Dhahabu wa Geita (GGM) kuwalipa fidia wananchi wanaoishi ndani ya
eneo la leseni ya Mgodi huo au kuwaruhusu rasmi waendelee kuishi humo na
kufanya shughuli za kiuchumi.
Sambamba na agizo hilo, pia
Serikali imeupa Mgodi huo siku 14 kuziba Tuta lililopasuka ambalo huzuia
maji machafu kutoka Mgodini yasiende katika makazi ya wananchi.
Aidha, kufuatia taarifa
iliyowasilishwa na timu ya wataalam wa mitetemo kutoka Wakala wa
Jiolojia Tanzania (GST), baada ya kukamilisha kazi waliyopewa kutafiti
chanzo cha mipasuko ya baadhi ya nyumba za wananchi na majengo
mbalimbali yaliyo jirani na Mgodi wa GGM, Serikali imeagiza timu hiyo
kufanya tathmini maalum ya idadi ya waathirika.
Iliagizwa kazi hiyo ifanyike kwa
kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Kitengo cha Maafa na Kitengo
cha Mazingira pamoja na uongozi kuanzia ngazi za vijiji mpaka madiwani
na wabunge husika kwa muda wa siku Saba tu kuanzia tarehe 29 mwezi huu
na kuiwasilisha serikalini ili hatua stahiki zichukuliwe.
Maagizo hayo yalitolewa hivi
karibuni mjini Geita na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard
Kalemani katika kikao chake kilichomshirikisha Mkuu wa Mkoa wa Geita na
wawakilishi wa wananchi wa Geita wakiwamo wabunge na madiwani.
Dkt Kalemani alisema kuwa maagizo
hayo ni kufuatia maelekezo aliyoyatoa mapema mwezi Februari mwaka huu
alipotembelea mkoani humo na kusikiliza kero za wananchi wa vitongoji
vya Katoma na Nyamalembo. Alisema maagizo hayo yasipotekelezwa ipasavyo
hatua kali za kisheria zitachukuliwa, chini ya sheria ya madini na
sheria nyingine za nchi.
Akifafanua zaidi kuhusu masuala
hayo yaliyosababisha Serikali kufikia hatua husika, Naibu Waziri alisema
kuwa mwezi Februari alipotembelea Geita, wananchi walieleza kero kubwa
walizokuwa nazo kuwa ni baadhi ya nyumba zao kupasuka kiasi cha kutoweza
kukalika na nyingine kukalika lakini zimeharibika kutokana na ulipuaji
wa baruti (blasting) wa Mgodi wa GGM.
Malalamiko mengine yalihusu
wananchi ambao wanaendelea kuwa na makazi ndani ya eneo la leseni ya
GGM, ambayo ina ukubwa wa kilomita za mraba 196. 7 ambao walikuwa
wanadai fidia ili waondoke katika eneo husika au waendelee kubaki na
kufanya shughuli zao za maendeleo.
Pia, baadhi ya wananchi wanaoishi
karibu na Mgodi na hasa maeneo ya chini ya Mgodi, walilalamikia maji
machafu ambayo yalikuwa yanakingwa na tuta ambalo lilikuwa limebomoka na
kuruhusu maji kutiririka kuelekea kwenye makazi yao na hivyo kuwepo
uwezekano wa kuathiri afya zao. Walitaka hatua madhubuti zichukuliwe
kuzuia mtiririko huo wa maji.
Alisema kuwa, baada ya kusikiliza
maelezo ya pande zote mbili, kwa suala la mipasuko, aliunda timu ya
wataalam wa Serikali kutoka GST na kuiagiza kufanya utafiti wa kisayansi
ili kubaini chanzo cha mipasuko husika kwa kushirikiana na wawakilishi
wa wananchi wa maeneo hayo.
Timu hiyo ilikamilisha kazi hiyo
na kukabidhi taarifa yake kwa Serikali mwezi Julai mwaka huu ambapo
ilibainisha vyanzo vikuu viwili vya mipasuko hiyo kuwa ni udhaifu wa
majengo yaliyoathirika lakini pia milipuko inayofanywa na GGM hasa ya
miaka ya nyuma hususan kuanzia mwaka 2007 hadi 2010 ambayo ilikuwa na
kipimo cha juu cha mitetemo kinachofikia 57.
Kuhusu wananchi wanaoishi kwenye
eneo la leseni, Dkt Kalemani alisema kuwa alimwagiza Afisa Madini wa
Geita kuwaandikia GGM ili wathibitishe kwa maandishi kati ya kuwaondoa
wananchi wale kwa kuwafidia kama eneo hilo lilivyo kwenye leseni yao au
kuwaruhusu waendelee kuishi na kufanya shughuli za maendeleo, jambo
ambalo Mgodi haukutekeleza badala yake walisema wananchi hao ni
wavamizi.
Aidha, kuhusu suala la Tuta,
Naibu Waziri alieleza kuwa, aliagiza lizibwe mara moja ili kuepusha
madhara ambayo yangeweza kujitokeza kama maji yangeendelea kutiririka
kuelekea kwenye makazi ya wananchi, ambalo pia halijatekelezwa hadi
sasa.
“Ni kutokana na hali hiyo, sasa
Serikali tumeona tutoe maagizo ya mwisho ili yatekelezwe na
yasipotekelezwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa.”
Naibu Waziri alisema kuwa
Serikali haina nia mbaya kwa Mgodi husika isipokuwa ni wajibu wa
Serikali kuhakikisha pia sheria zinafuatwa ili pande zote zipate haki
stahiki.
“Tunapenda sana wawekezaji muwekeze kwa sababu ndiyo mnatupa ajira, mnalipa mirabaha na kodi lakini lazima tuzingatie sheria.”
Dkt Kalemani alizitaka Mamlaka zinazohusika kusimamia zoezi hilo kikamilifu.
No comments:
Post a Comment