Wednesday, 3 August 2016

Mipango ya Pluijm dhidi ya MO Bejaia

Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amepanga kurejesha imani na furaha iliyopotea kwa mashabiki wa timu hiyo kwa kuhakikisha wanawafunga MO Bejaia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hiyo iliyopo mkiani katika Kundi A, ikiwa na pointi moja, imepoteza michezo mitatu na kutoka sare mmoja kati ya michezo minne iliyocheza.
Hata hivyo, kipigo kilichoshtua zaidi ni cha mabao 3-1 ilichokipata dhidi ya Medeama, hivi karibuni.
Yanga inatarajiwa kuvaana na MO Bejaia Agosti 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wake wa tano.

Pluijm amesema matokeo mabaya wanayoendelea kuyapata yanawakatisha tamaa mashabiki na kusababisha imani na timu yao kupungua.

"Tupo 'serious' hivi sasa katika maandalizi ya mechi yetu na MO Bejaia ambayo siyo ndogo kwetu, licha ya ugumu uliopo, lakini tutapambana kuhakikisha tunawafunga MO Bejaia.

"Ninajua imani ya mashabiki imepotea kwa kiasi kikubwa, hivyo nilichopanga ni kuirejesha kwa kuifunga MO Bejaia hapa nyumbani ili watoke uwanjani nao wakifurahia.

"Hilo linawezekana na nitahakikisha mashabiki wa timu hii wanakuwa na furaha, nimeshazungumza na wachezaji wangu na kuwaambia kuwa tunatakiwa kuwapa furaha mashabiki,” alisema Pluijm.

No comments:

Post a Comment