TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi nchini linapenda
kuutaarifu umma kwamba linatarajia kuwaaga Makamishna wa Jeshi la Polisi
watatu (3), ambao wamefikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria kwa
kutimiza miaka sitini (60) katika utendaji wao wa kazi.
Makamishna hao waliostaafu
Julai, 2017 ni pamoja na aliyekuwa Kamishna wa Polisi Operesheni na
Mafunzo, Paul Chagonja, aliyekuwa Kamishina wa Polisi Zanzibar, Hamdani
Omari Makame na aliyekuwa Kamishina wa Tume ya kudhibiti dawa za
kulevya Kenneth Kasseke.
Hafla hiyo itafanyika siku ya
Ijumaa tarehe 18/08/2017 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es
salaam (DPA), kilichopo barabara ya Kilwa, jijini Dar es eSalaam kuanzia
Saa Moja (7.00) Asubuhi. Wananchi wote pamoja na waandishi wa habari
mnakaribishwa.
Katika utumishi wao uliotukuka
ndani na nje ya Jeshi la Polisi walishika nyadhifa mbalimbali na
kuliletea sifa Jeshi la Polisi ndani na nje ya nchi. Kama tunavyofahamu
kuwa uhalifu hauna mipaka, wameshiriki kikamilifu katika operesheni
mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Kutokana na mchango wao kwa
taifa wametakiwa kuendelea kuwa msaada kwa Jeshi la Polisi wakati wowote
watakapo hitajika kutoa ushirikiano wa namna yoyote ili kusaidia
kupunguza uhalifu hapa nchini kwasababu suala la usalama ni taaluma kama
zilivyo taaluma zingine, na taaluma hiyo wanayo watu wachache.
Aidha, tunaamini watakuwa
mabalozi wa Jeshi la Polisi Tanzania hususani katika kipindi hiki cha
ushirikishwaji wa wananchi katika suala la ulinzi na usalama nchini
mahali popote watakapokuwa wakiendelea na shughuli zao za kila siku
baada ya kustaafu.
Imetolewa na:-
Barnabas David Mwakalukwa – ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment