WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka watu wote wenye nia ya kutaka kuwekeza katika miradi
mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na
taratibu.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Agosti 29, 2017) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa
Rais (Uendelezaji Bishara) wa kampuni ya PIRIOU, Bw. Michel Perrin.
Waziri Mkuu amekutana na Bw.
Perrin jijini Paris nchini Ufaransa kupitia ofisi ya ubalozi wa Tanzania
nchini Ufaransa. Kampuni ya PIRIOU inataka kuja nchini kuwekeza katika
utengenezaji na ukarabati wa meli.
Akizungumza na muwekezaji huyo
Waziri Mkuu alimshukuru kwa nia yake ya kutaka kuwekeza nchini, ambapo
alimtaka afuate sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji nchini.
“Tanzania ni sehemu nzuri ya
uwekezaji kwa sababu kuna fursa nyingi. Pia ni nchi yenye amani na
utulivu wa kisiasa pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo
nakukaribisha sana.”
Kwa upande wake Bw. Perrin amesema
ameamua kuja kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi salama na kwamba
anauhakika wa kupata soko ndani ya nchi pamoja na mataifa jiraji.
Amesema anaamini uwekezaji wake
nchini Tanzania utakuwa na tija, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa
ushirikiano wa karibu na Serikali na pia atahakikisha anafuata sheria
zote za nchi.
Pia Bw. Perrin alitumia fursa hiyo
kumshukuru Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Balozi Samwel Shelukindo
kutokana na ushirikiano anaompa kuhusu masuala ya uwekezaji nchini.
Naye Balozi Shelukindo amesema
atahakikisha anaendelea kutafuta wafanyabiashara mbalimbali na
kuwashawishi waje kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment