Na Mwandishi Wetu-MAELEZO
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango amesema serikali inathamini mchango wa sekta binafsi na
itaendelea kushirikiana nayo katika kuhakikisha azma ya Tanzania ya
viwanda inafikiwa.
Dkt. Mpango alisema hayo Jijini
Dar es Salaam leo alipokuwa akizindua kitabu cha Safari ya Tanzania
kuelekea katika Uchumi wa Viwanda 2016- 2056, kilichoandikwa na
watanzania wazalendo Bw. Ali Mufuruki, Gilman Kasiga na Moremi Marwa.
‘’Kitabu hiki ni kama mkombozi kwa
sisi watunga sera kwani kitatusaidia katika kuyafanyia kazi mapendekezo
ambayo yametolewa ili kuhakikisha Tanzania ya viwanda inawezekana,
nimewaelekeza pia Tume ya Mipango na Idara ya sera katika Wizara ya
Fedha kuchukua mapendekezo ambayo wataona yataisaidia serikali katika
kutekeleza azma yake ya kuendeleza viwanda’’alisema Dkt. Mpango
Bw. Ali Mufuruki mmoja wa watunzi
wa kitabu hicho alisema wameamua kuunganisha mawazo yao pamoja na
kutumia utaalamu na uzoefu wao katika masuala mbalimbali ya maendeleo na
uchumi ili kuisaidia serikali kuweza kuondokana na uchumi unaotegemea
kilimo na hatimaye kuwa nchi ya viwanda.
‘’Kuna changamoto nyingi
zinazozikabili nchi zinazoendelea ikiwemo ukosefu wa utaalamu katika
kilimo cha kisasa, ukosefu wa mitaji pamoja na kutokuwa na teknolojia ya
kutosha hivyo kwa kuwa azma ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni
kuwa na nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda, tukaona tumuunge
mkono katika kutimiza ndoto hiyo kwa kuandika kitabu hiki’’ alisema
Mufuruki.
Bw. Mufuruki alisema kuna mambo
mengi mazuri ya kulisaidia taifa ambayo yameainishwa katika kitabu hicho
hivyo ni vyema watanzania wa kawaida, wasomi, wachumi na hata
wawekezaji wakakisoma ili kuona kila mmoja katika nafasi yake anawezaje
kuisaidia nchi kutoka hapa ilipo na kufikia katika malengo iliyojiwekea.
Kwa upande wake Bw.Gilman Kasiga
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya General Electric katika ukanda wa
Afrika Mashariki, alisema ni vyema Tanzania ikawekeza katika masomo kwa
kutambua vipaumbele kama inavyofanya nchi ya Ujerumani ambapo sio kila
anayesoma ni lazima afikie ngazi ya shahada ndipo aonekane anaweza
kuleta mchango katika maendeleo.
Bw. Kasiga alisema asilimia 70 ya
wanaomaliza shule hapa nchini wanakimbilia kusoma shahada na kusahau
kwamba kuna masomo mengine katika ngazi za astashahada na cheti ambayo
kama yakifundishwa kwa umakini na kwa kuzingatia fani husika yanaweza
kuzalisha wataalamu wengi ambao wataisaidia nchi kupiga hatua
kimaendeleo na pia wao kupata ajira kwa urahisi katika viwanda.
Alisema elimu ya vyuo vikuu ni ya
kuandaa wasimamizi yaani mameneja na sio watendaji au wafanya kazi na
mafundi hivyo ameshauri mitaala ya vyuo iendane na ukuaji wa viwanda ili
wataaalamu hao waweze kutumia taaluma zao katika kulitumikia taifa.
No comments:
Post a Comment