Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigala King (katikati), akiongoza kikao
cha Kamati yake na Shirika la Posta Tanzania (TPC), kilichofanyika mjini
Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwin Ngonyani na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi
S. Kakoso.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akifafanua jambo kwa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu katika kikao chao na Shirika la Posta Tanzania
(TPC), kilichofanyika mjini Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Mhe. Prof. Norman Sigala King na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Sekta ya Mawasiliano Eng. Angelina Madete.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la
Posta Tanzania (TPC), Luteni Kanali mstaafu Haruni Kondo, akitoa taarifa
ya Shirika hilo kwenye kikao chao na Kamati ya Bunge ya Miundombinu
kilichofanyika mjini Dodoma. Kulia kwake ni mjumbe wa Kamati hiyo Mhe.
Anna Lupembe.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Mhe. Anna Lupembe (wa kwanza kulia), akichangia hoja katika
kikao cha Kamati hiyo na Shirika la Posta Tanzania (TPC), kilichofanyika
mjini Dodoma. Kushoto kwake anayesikiliza ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Shirika hilo Luteni Kanali mstaafu Haruni Kondo.
Shirika la Posta Tanzania (TPC),
limefanikiwa kukusanya madeni ya muda mrefu kutoka kwa taasisi za
Serikali, mashirika ya umma na sekta binafsi kiasi cha shilingi bilioni
7.6.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani katika kikao cha
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu
ya Shirika hilo kilichofanyika mjini Dodoma ambapo amesema makusanyo
hayo ni kati ya jumla ya shilingi bilioni 12 ambazo Shirika hilo linadai
wateja wake kuanzia mwaka 2011 hadi mwezi Juni mwaka huu.
“Hakikisheni mnamalizia makusanyo
ya deni lililobaki, kwani Shirika linahitaji kuendelea na kupata faida
kupitia makusanyo haya”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigala King ameiomba
Serikali kuliondoa Shirika hilo kwenye orodha ya mashirika yanayotaka
kubinafsishwa.
Ameongeza kuwa Serikali
ikitekeleza jambo hilo, italiwezesha Shirika hilo kujiendesha
kibiashara, kuzalisha faida na kukabiliana na changamoto za ushindani
kwenye soko.
Aidha, amelitaka Shirika hilo kuwa
wabunifu katika utoaji wa huduma zake kwa wananchi kwa kutumia
Teknolojia za kisasa zaidi badala ya kutumia mifumo ya kizamani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi
wa Shirika hilo Luteni Kanali mstaafu Bw. Haruni Kondo, ameiomba Kamati
hiyo kuendelea kushirikiana na Shirika hilo na kulisaidia ili liweze
kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
Taasisi za Serikali na Mashirika
ya Umma yanaendelea na utekelezaji wa agizo la Rais wa Awamu ya Tano wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya
kuhakikisha kuwa yanajiendesha kwa faida, kuongeza ukusanyaji wa mapato
na kudai madeni ya muda mrefu ili fedha hizo ziweze kutumika kuwahudumia
wananchi katika nyanja mbalimbali kama vile za elimu, afya na ujenzi wa
miundombinu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment