Na Said Ameir-MAELEZO
Serikali imesema kuwa viwanda
vingine 42 vitaunganishwa na mfumo wa matumizi wa matunizi ya gesi
asilia katika kipindi cha miaka miwili ili kuongeza tija tofauti viwanda
37 vya sasa ambavyo tayari vinatumia gesi hiyo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini
Dk. Medard Kalemani aliiambia Kamati ya Fedha ya Bunge jana kuwa
Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto zinazokwaza zoezi la
kuvipatia viwanda nishati hiyo zinatatuliwa haraka.
“Tuna gesi ya kutosha futi za
ujazo trilioni 57.25 ambapo hadi sasa tunatumia wastani wa futi za ujazo
milioni 70 ikiwa ni kama asilimia kumi tu hivi” alieleza Waziri
Kalemani
Kwa hivyo alisema azma ya Serikali
ni kuona viwanda vinatumia gesi katika uzalishaji na kubanisha kuwa
Tanzania inaongoza kwa kuwa na nishati hiyo katika Afrika Mashariki.
Waziri Kalemani aliieleza kamati
hiyo kuwa hivi sasa wateja wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda lakini
Serikali ipo mbioni kutekeleza mkakati wa kusambaza gesi hiyo kwa ajili
ya matumizi ya nyumbani.
Katika maelezo yake kwa kamati
hiyo ambayo ilitembelea kituo cha kupokelea gesi asilia huko Kinyerezi
na miradi ya uzalishaji umeme kwa kutumia gesi hiyo ya Kinyerezi I na
Kinyerezi II, Naibu Waziri huyo alidokeza kuwa Serikali ina mpango wa
kuanzisha kiwanda cha kusindika gesi asilia ili iweze kusafirishwa nchi
za nje.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha
ya Bunge Hawa Ghasia ameitaka TPDC kutayarisha mpango maalum kwa
kuainisha na kutenga maeneo maalum ambayo yatawekewa miundombinu ya gesi
ili uwekezaji wa viwanda uzingatie ramani hiyo.
“Tungetengeneza kanda maalum
tukaziandaa kwa ajili ya viwanda kwa kuziwekea miundombinu ya gesi
tofauti na sasa ambapo serikali inalazimika kuvifuata viwanda viliko
kuvipelekea nishati hiyo” alishauri Mwenyekiti huyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa shirika hilo lina nafasi ya pekee katika
kuifanya Tanzania kufikia lengo lake la kuwa nchi ya viwanda kama
itatekeleza vyema miradi ya matumizi ya gesi viwandani.
Aliueleza uongozi wa TPDC na
waandishi wa habari walioambatana katika ziara hiyo kuwa madhumuni ya
ziara ya kamati yake katika miradi hiyo ni kuangalia utayari wa shirika
hilo katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa viwanda bila ya vikwazo.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa
kamati yake imeridhika na kazi inayofanyika hadi sasa na kueleza
matumiani ya kamati yake kuwa miradi ya Kinyerezi I na Kinyerezi II
itamalizika kwa wakati na kufikia malengo yaliyowekwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TPDC Mhandisi Kapulya Musomba mpango wa shirika lake sasa ni
kutekeleza programu yake ya kusambza gesi nchi nzima kwa kuanzia na
mikoa ya Arusha, Mbeya, Mwanza na Tanga.
Alisema shirika lake lipo tayari
kukipatia kiwanda au mwekezaji nishati hiyo katika sehemu yeyote ambayo
bomba la gesi hiyo limepita na kwamba ingependeza kuona Tanzania ina
viwanda vingi ili gesi yote iweze kutumika humu nchini pasi na
kusafirishwa nchi za nje.
Mapema akijibu maswali kutoka kwa
wajumbe wa Kamati hiyo, Mhandisi Musomba alisema shirika lake linatumia
mifumo miwili ya usalama wa bomba lenye urefu wa kilomita 551
linalosafirisha gesi kutoka Mtwara hadi eneo hilo.
Aliitaja kuwa ni mfumo
unaojitegemea wa bomba hilo ambapo zinapotokea hitilafu hujizima na
wataalamu hufuatilia kuelewa hitilafu iliopo na mfumo wa pili ni ulinzi
shirikishi ambao wanawatumia wananchi kulinda bomba hilo.
Mbali na viwanda 37 kuunganishwa
katika mfumo wa matumizi ya gesi, shirika hilo pia limeziunganisha
familia 70 katika mfumo wa matumizi ya gesi hiyo katika maeneo ya
Mikocheni jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment