TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
28/08/2017
TUKIO LA MLIPUKO KWENYE OFISI ZA MAWAKILI WA IMMA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 26/8/2017 lilitoa taarifa
ya awali ya tukio la mlipuko uliotokea katika ofisi za mawakili wa IMMA
zilizopo katika eneo la Upanga jijini Dar Es Salaam.
Hivyo Jeshi la Polisi linapenda kuufahamisha umma kuwa uchunguzi wa
awali uliofanyika umebaini kwamba usiku wa kuamkia tarehe 26/8/2017
majira kati ya saa 7:00-8:00 watu wasiojulikana utambulisho wao na idadi
kamili, walifika katika ofisi za mawakili wa kampuni ya IMMA (IMMA
ADVOCATES) wakiwa na magari mawili wakijifanya ni askari na kuwarubuni
kisha kuwachukua walinzi wa jengo hilo na kuondoka nao kwenye moja ya
gari walilokwenda nalo,ambapo baadaye walinzi hao walikutwa maeneo ya
Kawe wakiwa hawajitambui.
Aidha, kundi lililobaki liliingia ndani ya Ofisi hizo na kuweka milipuko
iliyotengenezwa kienyeji ambayo baada ya watu hao kuondoka ililipuka na
kusababisha uhalibifu wa mali na jengo la ofisi hiyo pamoja na majengo
ya jirani.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa
linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini watu hao waliofanya
tukio hilo pamoja na kujua dhamira yao ili wakamatwe na kufikishwa mbele
ya sheria.
Aidha tunapenda ifahamike kuwa wajibu wa Jeshi la Polisi ni kulinda
maisha ya watu na mali zao hivyo kamwe haliwezi kutumika kuhujumu
maisha ya watu na mali za wananchi.
Tunaomba waathirika wa tukio hili na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu
wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi wa tukio. Vilevile,
tunatoa rai kwa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia katika
upelelezi waziwasilishe kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi.
B.M. KITALIKA- SACP
KAIMU KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment