Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo katika kikao na
Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko
wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kushoto ni Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Kakoso na kulia ni Naibu Katibu
Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara hiyo Eng. Angelina Madete.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina
Madete akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu
kuhusu miradi ya maendeleo ya mawasiliano vijijini katika kikao
kilichofanyika mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kasoso, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa
Kamati hiyo katika kikao kilichowakutanisha na uongozi wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
(UCSAF) mjini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng.
Edwin Ngonyani.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu Mhe. Dua Nkurua, akitoa maoni kuhusu ufikishaji wa
mawasiliano vijijini kwa viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (hawapo pichani) katika kikao na Kamati hiyo mjini Dodoma.
Kushoto kwake ni Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Bhagwanji Meisuria na kulia
ni Katibu wa Kamati hiyo Bw. Richard Masuke.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga akiwaonesha wajumbe wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu maeneo ya vijijini yaliyofikiwa na
mawasiliano katika kikao na Kamati hiyo mjini Dodoma. Kulia ni Mhe. Dua
Nkurua na kushoto ni Mhe. Rita Kabati wajumbe wa Kamati hiyo.
Serikali imesema kuwa imetumia
shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini kupitia Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za
mkononi ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za
mawasiliano.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani wakati akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenye
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu mjini Dodoma.
“Mfuko huu unaendelea kuhakikisha
kuwa mawasiliano bora yanafika katika maeneo mengi nchini hususan
vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara ambapo
Takwimu zinabainisha kuwa, tayari mawasiliano yamefikishwa kwenye kata
443, vijiji 1,939 kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Julai mwaka huu”,
amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.
Ameongeza kuwa tayari Mfuko
umetiliana saini mkataba na kampuni za simu za mkononi mwezi Agosti
mwaka huu kuhakikisha kuwa zinapeleka mawasiliano kwenye kata nyingine
75 na vijiji 154.
Aidha, ametanabaisha kuwa hadi
hivi sasa asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma ya mawasiliano nchini
na kuongeza kuwa, Serikali kupitia mkataba wake na Kampuni ya Simu ya
Halotel imefikisha mawasiliano kwenye jumla ya vijiji 3,069 kati ya
vijiji 4,000 tangu walipoanza utekelezaji wa jukumu hilo mwezi Novemba,
2015 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Novemba mwaka
huu.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso,
amezitaka kampuni za simu za mkononi zinazopeleka mawasiliano vijijini
na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ambazo zinapatiwa ruzuku na
Serikali kuhakikisha kuwa zinatoa taarifa sahihi kwa Mfuko huo ikiwemo
hatua zilizofikiwa za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa
mawasiliano kwenye vijiji husika.
Amewataka UCSAF kujitangaza na
kuweka mabango yao kwenye minara yote nchini iliyojengwa kupitia ruzuku
ya Serikali ili kuwawezesha wananchi kutambua uwajibikaji wa Serikali
katika kufikisha mawasiliano kwa wananchi wake.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina
Madete, amesema kuwa Wizara kupitia UCSAF itahakikisha kuwa kila
mwananchi anafikiwa na mawasiliano kuendana na jukumu la msingi la Mfuko
huo la kufikisha mawasiliano kwa wote.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Eng.
Peter Ulanga, amewahakakikishia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Miundombinu kuwa Taasisi yake itashirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakiki kazi zilizofanywa na kampuni za
simu za mkononi za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano
kwenye vijiji mbalimbali nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment