Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anaondoka
nchini leo kwenda Pretoria Africa ya Kusini ambako atamwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli katika Mkutano
wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika utakaofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 19 na 20 Agosti,
2017.
Mkutano huo utapokea
na kujadili ajenda mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti wa SADC na Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa
Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama; Hali ya
Michango mbalimbali ya Nchi Wanachama na Kupokea taarifa ya Mwenyekiti
anayeondoka wa SADC Organ.
Pia Mkutano utapokea
taarifa ya Katibu Mtendaji wa SADC; Kupitia hali ya kiuchumi katika
Kanda ya SADC; Kuwasilisha Kaulimbiu ya Mkutano wa SADC; Taarifa kuhusu
Mfuko wa Maendeleo wa SADC; Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
Viwanda; Kuwezesha Chuo cha Elimu ya Sayansi na Teknolojia; Maombi ya
Serikali ya Comoro na Serikali ya Burundi kujiunga na SADC; Utekelezaji
wa Mabadiliko ya Kitaasisi ya Umoja wa Afrika na Mkutano wa Mshikamano
kati ya SADC na Saharawi ya Magharibi.
Mkutano huo
utatanguliwa na Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Troika Mbili ya SADC (SADC Double Troika Summit) tarehe 18 Agosti, 2017
ambao Tanzania itakabidhi nafasi ya uenyekiti kwa mwenyekiti mpya.
Double Troika inahusisha nchi wanachama sita ambao kwa sasa ni
Swaziland, Tanzania, Afrika Kusini, Angola, Botswana na Msumbiji. Katika
mkutano huo Mfalme Mswati III wa Swaziland atakuwa ndiye Mwenyekiti.
Ajenda kuu katika Mkutano huu ni kupokea na kujadili taarifa kuhusu hali
ya kisiasa, kiulinzi na kiusalama katika Kanda na hasa nchini DR Congo
na Lesotho.
Makamu wa Rais
amefuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa AfrikaMashariki,
Mhe. Balozi Dkt Augustine Mahiga, Waziri wa Viwanda Biashara na
Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijange, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Ashatu
Kijaji na watendaji wengine waandamizi Serikalini
Makamu wa Rais na ujumbe wake anatarajia kurudi nchini Agosti 21, 2017.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
17/8/2017
No comments:
Post a Comment