Na Jacquiline Mrisho na Bushiri Matenda – MAELEZO
Serikali imewapiga marufuku
mawakala wa forodha wanaogushi nyaraka kwa ajili ya kuingiza kemikali
kwani ni kinyume cha Sheria na pia wanaipotezea Serikali mapato.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar
es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Prof. Samwel Manyele
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uingizaji wa
kemikali nchini kutoka nje ya nchi.
Prof. Manyele amesema kuwa kwa
mujibu wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali nchini kila
anayeingiza kemikali anatakiwa awe amesajiliwa na kupewa hati ya usajili
huo vile vile anatakiwa kupata idhini ya wakala wa Maabara ya Mkemia
Mkuu wa Serikali kabla ya kuagiza mzigo wa kemikali nchini.
“Natoa onyo kwa mawakala wote
wa forodha wasiofuata taratibu zilizowekwa na Serikali hasa wanaogushi
nyaraka zenye lengo la kukwepesha Sheria na kukwepa kulipa kodi na tozo
mbalimbali za Serikali hivyo watakaokaidi hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Prof. Manyele.
Prof. Manyele amesisitiza kuwa
kuanzia Leo Agosti 17, 2017 hakuna mtu atakayeruhusiwa kujishughulisha
na shughuli za kemikali bila kuwa na hati ya usajili wa shughuli
anayoifanya pia hakuna atakayeruhusiwa kuagiza mizigo ya kemikali bila
kuwa na kibali.
Aidha, Prof. Manyele
alifafanua lugha elekezi zinazotakiwa kutumika katika kuweka lebo za
kemikali husika kuwa ni Kiswahili na Kingereza tu hivyo hakuna kemikali
itakayoruhusiwa kuingia nchini ikiwa imendikwa kwa lugha tofauti na
hizo.
Vile vile hakuna mdau
atakayeruhusiwa kushiriki tenda za ununuzi kwa ajili ya kuuza kemikali
bila kuwa na usajili kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Ofisi ya Mkemia Mkuu
inaendelea kukabiliana na changamoto za wadau wa kemikali kwa kuendelea
kuwaelimisha wadau kuhusiana na matakwa ya Sheria na Kanuni za uingizaji
wa kemikali nchini, kuchukua hatua za kisheria kwa wale wanaokiuka
matakwa ya Sheria na kanuni zake, kuboresha mifumo, vifaa na sehemu za
kufanyia kazi pia wakala inaendelea kufanya kazi kwa masaa 24 katika
siku saba za wiki.
No comments:
Post a Comment