WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya
Korosho utakaofanyika kwa siku mbili kuanzia Jumamosi, Mei 13, 2007,
mjini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya
Korosho (CBT) Hassan Jarufu, amesema ya kuwa Mkutano huo Mkuu wa Wadau
wa Tasnia ya Korosho utawajumuisha washiriki wapatao 600 na utafanyika
kwenye Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Dodoma.
“Kama tulivyokwishakueleza, Mkutano
huu Mkuu utafunguliwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa na
watakuwapo pia Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba,
Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa inayolima Korosho ya Lindi,
Pwani, Tanga, Mtwara na Ruvuma.
“Tumealika pia waheshimiwa Wabunge
wanaotoka katika Mikoa hiyo, wakulima wa Korosho na watendaji wa Vyama
vya Ushirika vya zao la Korosho. Mkutano huu utajadili kwa kina
changamoto zinazoikabili Tasnia ya Korosho nchini,” alisema Jarufu.
Mkutano huu Mkuu wa Wadau wa Tasniaya
Korosho unakuja katika wakati ambao Tasnia ya Korosho imepata mafanikio
muhimu katika msimu uliopita ambayo ni pamoja na kuweka udhibiti
uliosababisha Korosho nyingi kuuzwa kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi
Ghalani na hivyo kupunguza matumizi ya Kangomba, kipimo ambacho kwa muda
mrefu kimekuwa kikimnyonya mkulima.
Udhibiti huo ulisababisha makusanyo ya
Korosho kuongezeka kutoka tani 155, 244.645 msimu wa 2015/2016 hadi
tani 264, 887. 527 katika msimu wa 2016/2017.
Kadhalika, Mkutano huu Mkuu wa Wadau
wa Tasnia ya Korosho unafanyika katika wakati ambao bei ya Korosho
imepanda kutoka 2,800/= kwa kilo ya Korosho ghafi daraja la kwanza msimu
wa 2015/2016 hadi 4,000/= kwa kilo katika msimu wa 2016/2017.
Aidha, katika hatua inayolenga kupanua
kilimo cha Korosho nchini, CBT imekuwa, kuanzia Februari mwaka huu,
ikigawa bure miche ya mikorosho kwa wakulima ili waongeze uzalishaji wa
zao hilo.
Kwa mujibu wa Jarufu, kwa kuanzia, jumla
ya miche milioni 10 itagawiwa kwa wakulima wa Mikoa ya Lindi, Pwani,
Tanga, Mtwara na Ruvuma mwaka huu.
“ Tumeanza kugawa bure kwa wakulima
miche ya mikorosho. Tutafanya hivyo kwa miaka mitatu mfululizo kwa kila
mwaka miche milioni 10. Sisi tumeigharimia lakini wao tunawapa bure.
Tunataka waitunze mpaka ikue ili hatimaye tuongeze kwa kiasi kikubwa
uzalishaji,” anasema Jarufu.
No comments:
Post a Comment