Rais Donald Trump tayari anayo orodha ya watu 11 anaowafikiria katika
nafasi iliyoachwa wazi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(FBI), James Comey, aliyemfukuza kazi.
Taarifa ya Ikulu ya nchi hiyo, White House, imesema hayo na tayari Idara
ya Sheria imejiandaa kuanza usaili wa watu hao kuanzia jana.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Ikulu nchini humo, Sean Spicer, ametoa
muhtasari kwamba Rais Trump atachagua mtu kujaza nafasi mara moja wakati
atakapompata mtu anayekidhi vigezo muhimu vya kuiongoza FBI.
Hata hivyo, uteuzi huo utakuwa na uchunguzi wa kina kwa kuwa Comey
alifukuzwa wakati akiongoza FBI kuchunguza iwapo kulikuwako na
ushirikiano kati ya kampeni ya urais ya Trump na Russia mwaka 2016.
Wafuatao ni watu 11 ambao wanafikiriwa katika nafasi hiyo:
Ray Kelly
Awali alikuwa Kamishna wa Polisi wa Jiji la New York kwa muda mrefu kuliko mtu mwingine yeyote.
Mike Rogers
Ni mfanyakazi wa FBI ambaye ameshikilia pia nafasi ya Kiti cha Ubunge
cha Michigan mpaka 2015 na pia amewahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya
Usalama ya Bunge.
Alice Fisher
Fisher alikuwa Naibu mwanasheria mkuu wa kitengo cha Jinai cha Idara ya
Sheria, chini ya utawala wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, George W. Bush.
Trey Gowdy
Huyu ni mbunge kutoka Jimbo la South Carolina na pia aliwahi kuwa mwendesha mashtaka wa serikali kuu.
John Cornyn
Ni seneta wa chama cha Republican kutoka Jimbo la Texas na ni mwenye
nafasi ya pili katika wadhifa wake kwenye Baraza la Seneti. Kabla ya
hapo alikuwa mwanasheria mkuu wa Texas.
Paul Abbate
Amefanya kazi miaka mingi na FBI na hivi sasa anatumikia nafasi ya
mkurugenzi mtendaji msaidizi wa Kitengo cha Jinai, Mitandao, Majibu na
Huduma.
Michael Garcia
Alikuwa ni mwendesha mashtaka wa jiji la New York na hivi sasa
anatumikia nafasi ya Jaji Msaidizi katika Mahakama ya Rufaa ya New York.
John Suthers
Suthers ni mwanasheria mkuu wa zamani wa Jimbo la Colorado na sasa ni meya wa mji wa Colorado Springs, katika jimbo hilo.
Michael Luttig
Luttig ni wakili wa zamani wa Idara ya Sheria na Jaji wa mahakama ya rufaa.
Larry Thompson
Thompson alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa Marekani kati ya mwaka 2001
hadi 2003, wakati wa utawala wa Rais mstaafu George W. Bush.
Andrew McCabe
McCabe amekaimu ukurugenzi wa FBI katika kipindi cha wiki hii, baada ya Trump kumfukuza kazi Comey. Ni Naibu Mkurugenzi wa FBI.
No comments:
Post a Comment