Mkutano mkuu wa mwaka wa
Shirikisho la wakuu wa Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO)
unatarajia kufanyika Mei 24, 2017 mkoani Arusha chini ya mwenyekiti wa
Shirikisho hilo kipindi hiki ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania,
IGP Ernest Mangu.
Mkutano huo utatanguliwa na
mikutano ya kamati tendaji za SARPCCO kabla ya kufunguliwa rasmi Mei
24, 2017 na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu
Nchemba ambapo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya
kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya Operesheni za pamoja
katika kubaini na kukabiliana na makosa mbalimbali yakiwemo dawa za
kulevya, wizi wa magari, usafirishaji haramu wa binadamu na ugaidi.
Vilevile, mkutano huo utajadili
utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Upelelezi wa SARPCCO
pamoja na kamati tendaji za sheria, Mafunzo na kamati tendaji ya Jinsia
na watoto katika mkutano wao uliofanyika mwezi Machi mjini Bagamoyo.
Aidha suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo.
SARPCCO iliundwa mwaka 1995 kwa
lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini
mwa Afrika katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu. Shirikisho hilo
linaundwa na Nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana,
Malawi, Lesoto, Mauritius, DRC, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini,
Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Syshelis.
Imetolewa na:-
Advera Bulimba-ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment