Wakala wa Vipimo (WMA)
Tanzania imeendelea na zoezi la utoaji wa elimu pamoja na uhakiki wa
mizani kwenye makampuni mbalimbali ya wafanyabiashara Mkoani Mwanza
katika Wilaya za Kwimba, Magu, Misungwi na Sengerema ikiwa ni
maandalizi ya msimu wa Pamba.
Akizungumza na Meneja wa Wakala wa
Vipimo Mkoani Mwanza Bwana Hemed Kipengele alisema jumla ya mizani
448 tayari imekaguliwa kutokana na makampuni manne ambayo tayari
yamekagulisha mizani yake na imekutwa ikiwa sahihi ambayo ni ICK (T)
LTD ambao walikuwa a mizani 184, SM HOLDING wenye jumla ya mizani 85
pamoja na NYANZA COTTON ambao walikuwa na mizani 179. Meneje
aliongezea kuwa zoezi hili la utoaji elimu pamoja na uhakiki wa mizani
itakayotumika kununulia Pamba linaendelea kwa Mikoa yote inayolima
Pamba ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Tabora pamoja na Mara.
Bwana Kipengele alisema
wanatarajia kutembelea jumla ya vijiji 101 ambavyo vina jumla ya vituo
vya kuuzia Pamba 150 ili waweze kutoa elimu na kufanya kaguzi za
kushutukize kwa wanunuzi wa Pamba ili kuona kama mizani waliyopima na
ikaonekana ni sahihi itaendelea kununua Pamba ya wakulima kwa vipimo
sahihi.
Meneja Kipengele aliwasihi
baadhi ya wakulima wanaolalamikiwa kuweka maji, kokoto pamoja na mchanga
kwenye Pamba kwa ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja
sababu Sheria ya vipimo ipo na inafanyakazi kwa pande zote mbili muuzaji
na mnunuzi wote kwa pamoja hawatakiwi kufanya udanganyifu wowote katika
biashara.
Kipengele alisema Sheria ya
Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo kuhakiki na kupiga chapa
vipimo vyote vinavyotumika katika biashara pia Wakala wa Vipimo
imeongeza na uwekaji wa sticker kwa kipimo kitakachokuwa
tayari kimehakikiwa ili iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani
iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka husika.
Alisisitiza kuwa kwa wale
watakaobainika kuchezea mizani kwa ajili ya kuwaibia wakulima adhabu ni
kuanzia laki moja hadi milioni ishirini endapo mkosaji atakubali kosa,
endapo kesi itafikishwa mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa
kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa mshitakiwa atatozwa faini
kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au
vyote kwa pamoja. Lengo kuu ni kumlinda mlaji ili apate faida na
thamani ya kile alichozalisha na siyo kupunjwa na wafanyabiashara
wajanjawajanja.
Tunaimani Tanzania ya viwanda
itafanikiwa endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia matumizi ya
vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji
wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokeaji wa mazao, ufungashaji hadi
utumiaji wa mazao yenyewe , hivyo vyote vikizingatia matumizi ya vipimo
sahihi viwanda vingi vitaweza kupata malighafi za kutosha sababu mkulima
na mfanyabiashara kila mtu atakuwa na imani na mwenzake kupitia
matumizi ya vipimo sahihi. Msema kweli na mleta haki katika biashara ni
kipimo sahihi kilichohakikiwa na Wakala wa Vipimo wala siyo
vinginevyo.
No comments:
Post a Comment