Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan, anatarajia kufanya ziara rasmi ya siku tatu kuanzia tarehe 05
Juni, 2017 Mkoani Mara.
Kwa mujibu wa ratiba ya Mkoa, Mhe Samia atatembelea Wilaya ya Tarime,
katika Kituo cha Afya cha Nyamwaga kinachojengwa na wananchi kwa msaada
wa Mgodi wa Acacia North Mara.
Pia, Mhe. Makamu wa Rais atapata fursa ya kutembelea Bonde la Mto Mara
kunakokusudiwa kuanza kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
Mchana siku hiyo hiyo atafanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha
Bisarwi; katika eneo hilo kunakusudiwa kujengwa kiwanda cha sukari.
Aidha tarehe 6/6/2017 Mhe. Makamu wa Rais ataenda Wilaya ya Serengeti
ambapo ataweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Wilaya; mchana
atafanya Mkutano wa Hadhara katika Uwanja wa Mbuzi, Mugumu mjini.
Tarehe 7/6/2017 Mhe. Makamu wa Rais atakuwa Musoma ambapo ataweka jiwe
la msingi kwenye barabara ya km.9.9 inayojengwa kwa kiwango cha lami
katika Manispaa ya Musoma. Pia atatembelea kiwanda cha Samaki cha Musoma
Fish Processors (T) Ltd na kufanya Mkutano wa Hadhara katika uwanja wa
Mukendo Musoma Mjini.
Hii ni mara ya kwanza Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa na ziara rasmi Mkoani Mara.
Jamal Zuberi
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Mkoa wa Mara.
30/05/2017
No comments:
Post a Comment