Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye mkutano
wa mwaka wa 5 wa Chama cha Makatibu Mahususi Tanzania (TAPSEA)
uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Jakaya Kikwete
,mjini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria
Mkutano Mkuu wa Chama Cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) ambao mgeni
rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza Makatibu Mahsusi
nchini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na waache tabia ya kutoa
siri za ofisi zao kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati
anafungua mkutano wa Tano wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania katika
ukumbi wa Jakaya Kikwete Mji Dodoma.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema uadilifu na uaminifu ni njia pekee ya kuaminiwa na
viongozi wao hivyo ni muhimu kwa makatibu mahsusi nchini kufanya kazi
kwa bidii na ubunifu mkubwa katika maeneo yao ya kazi.
Makamu wa Rais pia amewahimiza
makatibu mahsusi kufanya tathmini ya utendaji wao wa kazi na wawe tayari
katika kujifunza mbinu mpya za utendaji zinazoendana na mabadiliko ya
teknolojia.
“Sote tunafahamu kuwa dunia
imekuwa ni kijiji kutokana na utandawazi unaoletwa na mifumo ya
teknolojia hivyo kutokana na mabadiliko haya hamna budi nanyi kubadilika
na kwenda na wakati ili msiangaliwe kwa mtazamo hasi wa kuwa wapiga cha
tu”
Kuhusu uanzishwaji wa Shahada ya
Uhazili, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewahakikishia makatibu
mahsusi kuwa Serikali imekubali kuanzisha shahada hiyo ambapo masomo
yake yataanza mwezi wa Tisa mwaka huu kwenye Chuo cha Utumishi wa Umma
Tanzania katika mikoa ya Dar es Salaam na Tabora.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amewahimiza makatibu mahsusi kuchangamkia fursa hiyo kwa ajili ya
kujiendeleza kielimu kwa kuzingatia kuwa elimu haina mwisho.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah
Kairuki amesema Serikali inafanyia kazi baadhi ya kero zinazowakabili
makatibu mahsusi ikiwemo kuboresha maslahi ya kada ya uhazili nchini.
Amesema lengo la Serikali ni
kuhakikisha kada hiyo pamoja na watumishi wengine wanapata maslahi bora
ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ufanisi kazi.
No comments:
Post a Comment