Sunday, 4 December 2016

Kassim Majaliwa amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti kubadilisha uongozi wa Kituo cha afya cha Levolosi

rg1a5833
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti  kubadilisha uongozi wa  Kituo cha afya cha Levolosi baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa kinatoa huduma mbovu kwa wagonjwa hususan ni kwa wajawazito.
Pia amewataka wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kujenga hospitali za wilaya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za rufaa.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Desemba 4, 2016)  wakati alipotembelea  Hospitali ya mkoa ya Mount  Meru, ambapo alisema
tatizo la msongamano wa wagonjwa hospitali za rufaa na hospitali nyingine ni lazima lipatiwe ufunguzi.
“Hatuhitaji kuwa na madaktari ambao wanasumbua wagonjwa. Daktari wa Mkoa hakikisha kile kinacholalamikiwa kule Levolosi kinatafutiwa ufumbuzi. Hapa Mount Meru hakikisheni mnaboresha mazingira ya vyoo kwenye wadi  za wazazi pamoja na kujenga sehemu ya kuoshea vyombo kwa wagonjwa, ” alisema.
Awali alipotembelea wodi ya kinamama wanaosubiri kujifungua, mmoja wa wagonjwa, Glory Paul Mkazi wa Olasiti alimweleza Waziri Mkuu kuwa mtoto wake alifia tumboni baada ya wauguzi na  madaktari wa kituo cha Afya cha Levolosi  kuchelewa kumpatia matibabu.
“Wakati nahudhuria kliniki nishaambiwa na daktari kuwa natakiwa kujifungua kwa njia ya upasuaji na siwezi kujifungua kwa njia ya kawaida nilimwambia nesi kuwa  natakiwa kufanyiwa upasuaji wakanikatalia na kunilazimisha nijifungue kwa njia ya kawaida ambapo ilishindikana na baada ya muda waliniambia kuwa mtoto amekufa na wananifanyia upasuaji ili kuokoa maisha yangu,” amesema.
.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia alisema amepokea maagizo ya Waziri Mkuu, ambayo yanalenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza kuwa awali alichukua hatua za kinidhamu kwa watoa huduma za afya kituoni hapo na ataendelea kusimamia nidhamu ya kazi ili kuondoa malalamiko kwa wananchi juu ya huduma za afya.
                                                           
 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, DESEMBA 4, 2016.

No comments:

Post a Comment