Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya
Rufaa ya Dodoma Dkt. Samwel Seseja (Wa Pili kushoto), akitoa taarifa ya
namna mfumo wa TEHAMA unavyofanya kazi katika hospitali hiyo kwa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo (kushoto), alipokagua matumizi ya TEHAMA
katika hospitali hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo (Wa
Pili kulia), akiwasili katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kukagua
utendaji wa mifumo ya TEHAMA katika hospitali hiyo. Wa Kwanza kushoto ni
Afisa TEHAMA wa hospitali hiyo ni Bi. Sylivia Urio.
Muonekano wa mifumo ya TEHAMA
iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambayo itawezesha hospitali
hiyo kutoa huduma kwa njia ya kisasa na kwa urahisi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bahi Bi. Rachel Chuwa, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt.
Maria Sasabo (kushoto).
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Maria
Sasabo, amezungumzia umuhimu wa taasisi za umma zilizo chini ya mradi wa
Benki ya Dunia kuhakikisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), iliyofungwa inafanyakazi mara moja ili kuongeza
tija na ufanisi katika kuhudumia wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake
ya kukagua ufanisi wa matumizi ya TEHAMA katika hospitali ya rufaa ya
Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Dkt. Sasabo
amewataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha mifumo hiyo inakamilika
na kuanza kazi mara moja.
“Hakikisheni ifikapo mwezi
Septemba mawasiliano yenu na huduma zenu zilizounganishwa kwenye mifumo
ya TEHAMA inafanyakazi ili kurahisisha utendaji na kuiongezea Serikali
mapato”, amesema Dkt. Sasabo.
Dkt. Sasabo amemtaka Kaimu Mganga
Mkuu wa hospitali ya rufaa ya Dodoma Dkt. Samweli Seseja, kuhakikisha
hospitali hiyo inakuwa na mfumo maalum wa mawasiliano utakaowezesha
kuboresha huduma katika hospitali hiyo na kumudu ongezeko la watu katika
Manispaa ya Dodoma.
Akiwa wilayani Bahi, Katibu Mkuu
huyo wa mawasiliano amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya
Bahi Bi, Rachel Chuwa kuhakikisha mifumo ya Tehama iliyofungwa katika
ofisi za halmashauri hiyo na katika shule za sekondari wilayani humo
inafanyakazi mara moja ili kuendana na malengo ya serikali katika utoaji
wa huduma bora, za kisasa na kwa wakati kwa wananchi wake na hivyo
kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025.
Serikali imekuwa ikihamasisha
matumizi ya TEHAMA katika taasisi zake zikiwemo ofisi, shule, hospitali
na vituo vya polisi ili kuboresha huduma na kuwezesha uwazi katika
ukusanyaji wa mapato na hivyo kuhamasisha wananchi kuchangia huduma kwa
hiari.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment