Mkuu wa Mkoa wa
Tabora Agrey Mwanri amesema kipaumbele cha uongozi wa mkoa wake ni
kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa vijana na wananchi wa mkoa huo
kuchangamkia kila fursa zitakazotajitokeza Mkoani humo wakati wa ujenzi
wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi mkoa
wa Tanga.
“Tunataka tuwaelimishe na
kuwahamasisha vijana, kinamama na wananchi wote wa mkoa wetu kuhakikisha
wanazitumia fursa zote zitakazojitokana na mradi huu ili waweze
kujiendeleza” alisema Mwanri na kuongeza kuwa uongozi wa mkoa wake hauko
tayari kuona vijana wanabaki kuwa watu wa kupiga makofi na kushangilia
tu.
Mkuu wa Mkoa Tabora alisema hayo
wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu katika kijiji cha
Chongolieni Mkoani Tanga mara baada ya kuhudhuria hafla ya uwekaji wa
jiwe la msingi la mradi huo uliofanywa kwa pamoja na Marais wa Uganda
Yoweri Kaguta Museveni na Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
Aliongeza kuwa jambo muhimu
watakalolifanya ni kuhakikisha kuwa vijana wa Mkoani wa Tabora
wanashirikiana kikamilifu na wataalamu ambao watakuwa wakijenga
miundombinu ya mradi huo pamoja na kutoa huduma zitakazohitajika ili
waweze kufaidika na fursa hiyo za mrai huo.
“Tunauangalia mradi huu kuwa ni
fursa nyingine ya kipekee ya kuzidi kuufungua mkoa wetu kiuchumi kwa
kuzidi kujenga mazingira mazuri ya kuvutia biashara na uwekezaji”,
alisisitiza Mkuu wa Mkoa huyo.
Alifafanua kuwa uwekezaji kwa
kawaida una sura nyingi unaweza kuleta mitaji, tekinolojia, kuongeza
ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
Bwana Mwanri alieleza kuwa kwa
uongozi na wananchi wa Tabora wanaona fahari kwa jambo kubwa kama hilo
la kihistoria linafanyika katika Mkoa wao ambao bomba hilo litapitia
katika Wilaya za Igunga na Nzega.
“Sisi tumejipanga kunufaika vizuri
na mradi huu….si ni wakulima wa mpunga, maharage, viazi vitamu, maboga,
tikiti maji nk… hizi zote ni fursa zaidi kuinua biashara ya mkoa wetu”,
alisema.
Aliongeza kuwa kusema kuwa “Mkoa
unazidi kufunguka kwa kasi. Reli ya standard gauge inapita Tabora kwa
kilomita nyingi, ukienda Shinyanga, Mwanza, Itigi ukitaka kwenda Kigoma
tuko na barabara zetu nazo zinajengwa kuufungua mkoa”.
Mkuu wa Mkoa huyo wa Tabora
alifafanua kuwa ulinzi wa bomba hilo utapewa kipaumbele katika mkoa wake
na kubainisha kuwa wananchi ndio wakataokuwa walinzi wa awali wa bomba
hilo kwa kuwa wao ndio watakaoweza kuvieleza vyombo vya hujuma au
uharibifu utakapotokea ua unaodhamiriwa kufanywa dhidi ya bomba hilo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wakuu
wa mikoa nane ambayo bomba hilo litapitia ambayo ni Kagera, Geita,
Shinyanga, Singida, Manyara, Dodoma na Mkoa wa Tanga.
Bomba la hilo la mafuta ambalo litagharibu dola bilioni 3.5, asilimia 80 ya ujenzi wake utafanyika Tanzania.
No comments:
Post a Comment