Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP
Simon Sirro akisalimiana na Kamishna Mstaafu Paul Chagonja wakati wa
sherehe zilizoambatana na Gwaride maalumu la kuwaaga makamishna wastaafu
watatu, gwaride lililofanyika katika viwanja vya Chuo cha Maafisa wa
Polisi Dar Es Salaam ambapo wastaafu hao walisukumwa kwenye gari maalumu
na Makamishna Wasaidizi Waandamizi sita ikiwa ni utaratibu wa Jeshi
hilo katika kuwaaga maofisa wakuu. Kulia ni Kamishna Mstaafu Hamdani
Makame.
Kamishna Mstaafu Paul Chagonja
akikagua gwaride maalum lililoandaliwa kwaajili ya sherehe ya kuwaaga
makamishna wastaafu watatu akiwemo kamishna Chagonja, Kmaishna Paul
Chagonja na Kamishna Kenneth Kaseke. Gwaride hilo lilifanyika katika
viwanja vya Chuo cha Maafisa wa Polisi Dar Es Salaam ambapo wastaafu hao
walisukumwa kwenye gari maalumu na Makamishna Wasaidizi Waandamizi sita
ikiwa ni utaratibu wa Jeshi hilo katika kuwaaga maofisa wakuu.
Makamishna wastaafu Paul Chagonja
(kushoto) na Hamdani makame wakisukumwa kwenye gari na Makamishna
Wasaidizi Waandamizi sita ikiwa ni utaratibu wa Jeshi la Polisi katika
kuwaaga maofisa wakuu. Makamishna hao wamestaafu utumishi wa umma kwa
mujibu wa sheria na waliandaliwa Gwaride maalum la kuwaaga lililofanyika
katika viwanja vya Chuo cha Maafisa wa Polisi Dar Es Salaam
Picha kwa hisani ya Jeshi la Polisi
Na. Jeshi la Polisi.
Makamishna wastaafu wa Polisi Paul
Chagonja, Hamdan Omar Makame na Kenneth Kaseke wametakiwa kuendeleza
elimu ya Polisi jamii pamoja na kutoa msaada wowote utakaohitajika kwa
Jeshi la Polisi pindi wanapokuwa katika maisha ya uraia baada ya
kustaafu utumishi wa Jeshi la Polisi ili kuhakikisha kuwa wahalifu
hawapati nafasi ya kutamba hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini IGP Simon Sirro wakati wa sherehe zilizoambatana na
Gwaride maalumu la kuwaaga wastaafu hao lililofanyika katika viwanja vya
Chuo cha Maafisa wa Polisi Dar Es Salaam ambapo wastaafu hao
walisukumwa kwenye gari maalumu na Makamishna Wasaidizi Waandamizi sita
ikiwa ni utaratibu wa Jeshi hilo katika kuwaaga maofisa wakuu.
IGP Sirro alisema kazi
waliyofanya wastaafu hao ni kubwa lakini kustaafu kwao siyo mwisho wa
kutumika katika kazi za Polisi na hivyo waendelee kuwa tayari wakati
wowote kwa kuwa sasa Jeshi la Polisi linaendelea kushirikisha jamii
kukabiliana na uhalifu.
“Upolisi ni taaluma kama zilivyo
taaluma nyingine hivyo utaalamu hauzeeki na kwetu sisi tunaondelea
kubaki Jeshini tutaendelea kufuata yale yote mazuri mliyofanya na nyie
mnapokuwa nje ya utumishi endeleeni kutusaidia kwa mawazo na milango
yetu ipo wazi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama” Alisema IGP
Sirro
Akizungumza baada ya kuagwa rasmi
Jeshini Kamishna Paul Chagonja ambaye alikuwa Kamishna wa Oparesheni na
mafunzo kwa muda mrefu amewaasa Maofisa na Askari kuendeleza tamaduni na
maadili ya Polisi pamoja na kufanya kazi kwa weledi.
Chagonja amesema nidhamu ndio
msingi wa Askari Polisi popote pale wafanyapo kazi zao hivyo amewaomba
kuendelea kusimamia sheria bila ya kumuonea muhali mhalifu yeyote.
Kwa upande wake Aliyekuwa Kamishna
wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame amewashukuru wananchi wote
hususani wa Visiwani kwa ushirikiano waliompatia kipindi chote hali
ambayo imesababisha Zanzibar kuendelea kuwa shwari.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na
Viongozi mbalimbali kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, Mkurugenzi wa
Takukuru Kamishna Valentino Mlowola, IGP Mstaafu Said Mwema, DCI Mstaafu
Robert Manumba na Kamishna Mstaafu wa Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam
Suleiman Kova pamoja na maofisa na Askari Polisi.
No comments:
Post a Comment