Rooney ni kati ya wachezaji mahiri zaidi duniani kwa sasa akiwa na heshima kubwa kwenye soka la England.
Staa huyu amerejea kwenye kikosi cha Everton, ambacho alianzia hapo kabla hajaondoka na kujiunga na Manchester United ambayo ameitumikia kwa mafanikio makubwa.
Staa huyo amekuwa akitumika kama kielelezo cha ubora kwa wachezaji wengi vijana duniani kutokana na mafanikio ambayo ameyapata hadi sasa.
Kurejea kwake kwenye kikosi cha Everton kunaonyesha kuwa amerejea nyumbani kwake, sehemu ambayo alitumika kwa muda kabla hajajiunga na United.
Juzi mshambuliaji huyo ambaye aliifungia Everton bao kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Stoke, alisema kuwa yeye ni binadamu na anajua kuwa kuna mazuri aliyoyafanya kwenye kikosi cha United.
Rooney amewashangaza wengi aliposema kuwa anajua kuwa kuna watu wanaweza kuvunja rekodi yake kwenye timu ya United, lakini yeye duniani anawaona watu wawili tu ambao wanaweza kufanya hivyo.
Rooney ambaye ndiye kinara wa mabao kwenye timu hiyo, amesema mshambuliaji wa sasa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na staa wa sasa wa Barcelona, Lionel Messi, endapo mmoja wao anaweza kujiunga na United basi ndiye anaweza kuvunja rekodi yake.
Katika kipindi chake cha miaka 13 ambacho amekaa kwenye timu ya United, Rooney, amefanikiwa kuifungia timu hiyo mabao 253 katika michezo 253 idadi ambayo ni kubwa zaidi kwenye timu hiyo kwa sasa.
Rooney mwenye umri wa miaka 31, amesema kuwa kwa sasa itakuwa vigumu kumpata mchezaji anayeweza kuvunja rekodi hiyo kwa kuwa vijana wengi hawataki kukaa kwenye timu kwa muda mrefu.
Anasema kuna wachezaji wengi wa uwezo kwenye timu hiyo, lakini ukweli ni kwamba watashindwa kuvunja rekodi hiyo kwa kuwa hawapo tayari kukaa kwenye timu moja miaka kumi.
“Huwezi kujua kama United wanaweza kumpata mtu kama Ronaldo au Lionel Messi, ndiyo wanaweza kuvunja rekodi yangu.
“Lakini nafikiri kwa soka la sasa ni vigumu kwa mchezaji kukaa kwenye timu muda mrefu, hivyo kwa aina ya hawa waliopo itakuwa vigumu sana.
“Kwa hali ilivyo kwa sasa nafikiri ni vigumu kwa mchezaji kukaa kwenye timu kama enzi zetu, mtu akikaa United miaka minne au mitano hawezi kuvunja rekodi hii ya kucheza michezo 500 au kufunga mabao 200.
“Ni jambo zuri kuondoka kwenye timu ukiwa na rekodi kama hii, hili ni jambo zuri sana, niliondoka United na rekodi na nataka kuendelea kuishi nayo.
“Bado United ni sehemu ninayoipenda kwa kuwa nilifanya vizuri pale, lakini nafikiri ulikuwa umefika muda muafaka kwangu kuondoka kwenye timu hiyo kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.
“Pamoja na kufunga mabao lakini elewa pia kuwa nimefanikiwa kutwaa makombe nikiwa na timu hii jambo lingine ambalo ni zuri sana kwangu.
“Nina rekodi ya makombe ni lazima niiheshimu sana, lakini sikuwa nafuraha msimu uliopita ambao tulitwaa Kombe la Europa na Kombe la Ligi, lakini mimi najiona kuwa sikushiriki hata kidogo,” alisema Rooney.
Mshambuliaji huyo raia wa England alijiunga na United mwaka 2004, na kutumika hapo hadi mwaka 2017 alipoondoka na kurejea Everton alipoanzia soka.
Akiwa na United, mshambuliaji huyo amefanikiwa kutwaa makombe 15 akiwa ametwaa makombe yote makubwa likiwemo lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia ana rekodi nzuri kwenye timu ya Taifa ya England akiwa ameitumikia kwenye michezo 119 na kufunga mabao 53.
No comments:
Post a Comment