Tuesday, 1 August 2017

NEC yalitaka Gazeti la MwanaHalisi Kuomba Radhi

Image result for Ramadhani kailima
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
 

TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU TAARIFA ZA UONGO NA UZUSHI DHIDI YA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI ZILIZOTOLEWA NA GAZETI LA MWANAHALISI
Katika Maoni ya Mhariri ya Gazeti la MwanaHalisi Toleo Na. 402 la Jumatatu, tarehe 31 Julai – 06 Agosti, 2017, yenye kichwa cha habari “Kwa hili, NEC imechafuka zaidi”.
Maoni ya Mhariri wa gazeti hilo yameonesha kwa mara nyingine na kwa makusudi kabisa namna ambavyo gazeti hilo siyo tu haliandiki habari sahihi na za kweli kuhusu NEC bali kutokuwa makini katika uandishi na kutozingatia miiko ya taaluma ya uandishi wa habari, umakini na weledi wa Mhariri anayeandika maoni yasiyo na ukweli wowote.
Tume inapenda kukanusha uongo na uzushi huo kwa ufafanuzi ufuatao:
Mosi, majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi yamefafanuliwa vema kwenye Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, inaelezea majukumu ya Tume.
 Pili, kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 hakijaweka masharti kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hali ya migogoro kwenye Vyama vya Siasa na/au hali (status) ya mashauri yanayohusu migogoro hiyo yaliyofunguliwa Mahakamani. Kwa mantiki hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi si mamlaka ya kushughulikia masuala ya migogoro ya Vyama vya Siasa na mashauri yaliyoko Mahakamani yanayohusu migogoro hiyo.
Tatu, baada ya Spika kutekeleza mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kutangaza na kuijulisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi juu ya uwepo wa nafasi ya wazi ya Kiti cha Ubunge, Tume haina mamlaka Kisheria na Kikanuni ya kujielekeza katika migogoro ya Vyama vya Siasa na/au mashauri mbalimbali ya Vyama hivyo yaliyofunguliwa Mahakamani. Tume inao wajibu wa kujaza nafasi kama hizo kwa kuzingatia masharti yaliyo wazi ya vifungu 37 (3) na 86A vya Sheria ya Uchaguzi.
Nne, kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume hushauriana na Chama cha Siasa husika ili kishauri na kupendekeza majina ya wanachama wenye sifa za kuteuliwa katika nafasi ya Wabunge wa Viti Maalum kutoka katika orodha ambayo ilishaletwa na chama husika wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Tano, Tume ilikiandikia barua Chama cha Wananchi – CUF kuhusu uwepo wa nafasi hizo wazi. kwa kuzingatia masharti ya ibara 78(4) ya kifungu cha 86A(8) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, CUF walijibu kwa kushauri na kuwasilisha mapendekezo ya wanaofaa kuteuliwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum kutoka katika orodha ya majina waliyoiwasilisha wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Sita, kwa mujibu wa ibara 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na kifungu cha 86A(8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, majina nane (8) yaliyopendekezwa na CUF kujaza nafasi wazi za Wabunge wa Viti Maalum ni miongoni mwa majina hamsini na tano (55) yaliyowasilishwa na CUF kwa barua yenye Kumbukumbu nambari CUF/AK/DSM/KM/003/1A/2015/14 ya tarehe 28/09/2015 ambayo ilisainiwa na Katibu Mkuu wa CUF – Seif Sharif Hamad.
Saba, Tume katika kujaza nafasi wazi nane (8) za Wabunge Wanawake wa Viti maalum haikukiuka taratibu zozote za Kikatiba, Kisheria na Kikanuni. Aidha, utaratibu huu ndiyo uliotumika kujaza nafasi wazi ya viti maalum kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 14 Aprili, 2017 na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tarehe 04 Mei, 2017.
Nane, inasikitisha kuona Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi bila kuwasiliana na Tume ili kupata taarifa za kweli kuhusu utekelezaji wa majukumu yake, anazingatia taarifa za uzushi na uongo kutoka CUF na kuandika taarifa zisizo na ukweli na usahihi wowote kwamba, majina yaliyoteuliwa na Tume kuwa Wabunge wa Viti Maalum hayakutoka katika orodha iliyowasilishwa na chama husika mwaka 2015.
Tisa, kwa mujibu wa kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume hutakiwa kuitisha uchaguzi mdogo wa Madiwani mara mbili kwa kila mwaka ndani ya kalenda ya mwaka. Aidha, uchaguzi mdogo wa kwanza katika mwaka wa kalenda wa 2017 ulifanyika mwezi Januari, 2017.
Kumi, Aidha, chini ya masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria hiyo, Tume huitisha Uchaguzi Mdogo wa kujaza nafasi wazi za Madiwani iwapo itakuwa imepokea taarifa ya uwepo wa nafasi wazi kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa. Tume inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo wa madiwani wa Kata na kujaza nafasi wazi za Madiwani wa Viti Maalum baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa hivi karibuni.

Kumi na Moja, hivyo, siyo kila wakati inapotokea nafasi wazi ya Udiwani wa Kata ndani ya kalenda ya mwaka Tume itaitisha uchaguzi mdogo, inategemea na uzingatiaji wa kifungu cha 13(1)(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292
Kwa kuzingatia maelezo na ufafanuzi huo, madai ya Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi kwamba, Tume imeshindwa kutangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa nafasi za madiwani, hazina ukweli wowote, ni uzushi na uongo na zisizo na mashiko.
Hii siyo mara ya kwanza kwa gazeti la MwanaHalisi kuandika habari za uongo na uzushi dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mfano katika gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 322 la tarehe 18 – 24 Januari, 2016 liliandika habari za uongo na uzushi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Walipotakiwa kuomba radhi, waliomba radhi kwa kwa barua yenye Kumbukumbu nambari HHPL/ADM/01/02/16 ya tarehe 04 Februari, 2016 iliyosainiwa na Mhariri Mtendaji ambapo aliahidi kusahihisha katika gazeti la MwanaHalisi la tarehe 08 Februari, 2016 jambo ambalo walifanya.
Kwa kuwa, inaonesha dhahiri kwamba, Mhariri aliyeandika tahariri katika gazeti la MwanaHalisi hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu majukumu ya Tume na hakutaka kujishughulisha kujielimisha kujua ukweli halisi kabla ya kuandika tahariri yake; na
Kwa kuwa, uandishi wa aina hii siyo tu ni uandishi usiozingatia miiko ya taaluma ya uandishi wa habari, weledi na umakini; na
Kwa kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetumia fursa hii kutoa elimu na ufafanuzi sahihi kwa gazeti la MwanaHalisi.
 
Hivyo basi, inategemewa kwamba, baada ya taarifa hii, Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi kama alivyofanya awali aombe radhi kwa kutoa taarifa za uzushi na uongo. Aidha, inasisitizawa kabla ya kuandika taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume ni vema akawasiliana na Tume ili kupata taarifa sahihi.
Imetolewa leo tarehe 01 Agosti, 2017 na:

Kailima, R.K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI

No comments:

Post a Comment