Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akiwa na mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nnje
wa CUBA Bibi Ana Teresa mara baada ya kuwasili jana August 17/2017
katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Havana kwa ajili ya ziara ya
kikazi Nchini Cuba
Waziri Mkuu Kassim Majliwa na
Mkewe Mary Majaliwa wakipata makaribisho Nchini Cuba jana August 17/2017
kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nnje wa CUBA Bibi Ana Teresa mara
baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Havana kwa
ziara ya kikazi Nchini Cuba
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli
inayatambua na kuyathamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyojengwa
na awamu zilizotangulia baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali ikiwemo
Jamuhuri ya Cuba na kwamba itayaendelea.
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Alhamisi, Agosti 17, 2017), alipozungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje wa Cuba, Bi Anna Teressa mara baada ya kuwasili nchini Cuba kwa
ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya
nchi hizo mbili.
“Tanzania na Cuba zina historia ya
kutosha. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili,
ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi
wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere.”
Amesema katika ziara yake hiyo
anatarajia kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali waandamizi wa
Serikali ya Cuba kwa lengo la kukuza ushirikiano katika sekta za Afya,
Elimu, Utalii na Kilimo.
Waziri Mkuu amesema Cuba ni
mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania
kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.”Mfano katika Sekta ya Afya,
madaktari wengi kutoka Cuba walikuwa wanakuja Tanzania kutibu wagonja
waliokuwa na maradhi makubwa.”
Pia Waziri Mkuu amesema katika
ziara hiyo anatarajia kukutana na Jumuya ya Wafanyabiashara wa Cuba ili
kuwaelezea fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania hususan katika
Sekta ya Viwanda pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo
nchini.
Kwa upande wake Bi. Anna ambaye
alimpokea Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Cuba alitumia fursa hiyo
kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea ushirikiano mzuri baina ya
nchi hizo mbili, hivyo alimuhakikishia kwamba wataendelea kuudumisha.
Pia Bi. Anna ametumia fursa hiyo
kuupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John
Magufuli kwa namna inavyopambana na rushwa, ufisadi, kuhimiza
uwajibikaji pamoja na kutetea wanyonge.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 18, 2017.
No comments:
Post a Comment