Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
05/05/2017
Dar Es Salama.
WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania
(TEMESA) imeunda kikosi kazi maalumu kitakachohusika na zoezi la
ukusanyaji wa madeni ya kiasi cha Tsh Bilioni 10 inazodai TEMESA katika
taasisi za Serikali.
Hadi kufikia mwezi machi mwaka huu
TEMESA imekusanya kiasi cha Tsh milioni 157 inazodai kutoka katika
taasisi mbalimbali za Serikali.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji
Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu wakati wa mahojiano ya kipindi maalum
cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari- MAELEZO na kurushwa
hewani na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC).
Dkt Mgwatu alisema kuwa TEMESA ina
jukumu la kutoa huduma za kiuhandisi kwa Taasisi za Umma na watu
binafsi ikiwemo uzalishaji na utengenezaji magari pamoja na uboreshaji
mitambo na huduma za vivuko na huduma za ushauri na uendeshaji.
“TEMESA imekuwa ikiongeza vivuko
kulingana na mahitaji ya huduma hivyo ina mpango wa kuongeza kivuko
kimoja katika eneo la Kigamboni na kufanya vivuko kuwa vitatu
vitakavyofanyakazi saa 24 kwa lengo la kurahisisha huduma ya usafishaji”
alifafanua Dkt. Mgwatu.
Aidha alisema kuwa katika mwaka wa
Fedha 2017/2018 TEMESA imepanga kuboresha zaidi matumizi ya TEHAMA kwa
lengo la kurahisisha utendaji kazi ndani ya TEMESA na kuboresha huduma
ili kuwavutia taasisi na watu binafsi kupata huduma za taasisi hiyo.
Vilevile Dkt. Mgwatu aliongeza
kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka 2017 TEMESA imepanga kupunguza gharama za
tozo za utengenezaji wa magari kwa taasisi za umma na watu binafsi.
Mbali na hayo Wakala wa Ufundi na
Umeme nchini kwa mwaka 2016/2017 imeweza kutekeleza miradi mbalimbali
mikubwa iliyokamilika ndani ya muda uliopangwa ambapo imeshiriki pia
katika ujenzi wa Hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM).
No comments:
Post a Comment