Na Husna Saidi & Nuru Juma- MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kushughulikia suala
la huduma za afya bure kwa watu wenye ulemavu.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla kwa niaba ya Waziri Ummy
Mwalimu.
Akizungumza wakati wa kipindi cha
maswali na majibu kufuatia swali la Mbunge wa Viti Maalum Stella Ikupa
Alex aliyetaka kupata ufafanuzi juu ya suala hilo, Dkt. Kigwangalla
alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kutoa huduma za afya bure kwa
makundi maalum likiwemo watu wenye ulemavu.
“Dhumuni la Sera ya Afya ya mwaka
2007 ni kuwezesha watu wenye ulemavu wazingatiwe katika makundi maalum
ya watu wanaostahili msamaha utolewao kwa kuzingatia endapo mlemavu huyo
hana uwezo wa kulipia huduma hiyo au awe katika makundi maalum ili
kupata huduma bora za afya kama ilivyo kwa watu wengine,” alisisitiza
Dkt.Kigwangalla.
Sera hiyo imeainisha makundi
maalum yanayostahili kupata msamaha wa huduma za afya katika vituo vyote
vya kutolea huduma kuwa ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 60, watoto
chini ya miaka mitano,watoto waishio katika mazingira hatarishi,
wajawazito na watu wasiojiweza kiuchumi.
Aliongeza kuwa watu wengine ambao
wapo kwenye makundi maalumu ni wenye magonjwa sugu kama Kifua kikuu,
Ukimwi, Kisukari, Magonjwa ya Moyo, Pumu, Sikoseli, Ukoma, Saratani na
Magonjwa ya Akili.
Aidha alisema kuwa katika kuweka
uwiano sawa kwa Watanzania wote bila ubaguzi Serikali ya awamu ya tano
ina pendekezo la kutoa bima ya afya ya lazima kwa watu wote ambapo
utasaidia pia kwa watu wenye msamaha kupata huduma bora.
Kama Serikali itapitisha pendekezo
la kutoa bima ya afya ya lazima kwa Watanzania wote litasaidia
upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment