Na Daudi Manongi-MAELEZO, DODOMA.
Serikali imesema kuwa haina mpango
wowote wa kusitisha mbio za Mwenge wa Uhuru na kusisitiza kuwa dhana
hii ni endelevu na itaendelea kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa
kusisitiza misingi hii bila kuchoka.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi , Vijana , Ajira na wenye
Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama wakati akijibu hoja mbalimbali Mjini
Dodoma.
“Kutokana na faida na Mafanikio
makubwa yanayopatikana kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru Serikali inaamini
kuwa zipo faida nyingi ndani yake na mwenge huu utaendelea
kudumu”,Alisisitiza Mhe.Muhagama.
Amesema kuwa Kimataifa Mwenge wa
Uhuru umeendelea kusimamia dhana na maudhui yake ya kumulika hata nje ya
mipaka yetu kwa kuwa msuluhishi wa Amani Afrika na mfano wa kuigwa kwa
mataifa mengine Afrika na Dunia kote.
Aidha amesisitiza kuwa Umoja ,Mshikamano ,Upendo na Ukarimu wa Watanzania ni matunda ya Mwenge wa Uhuru.
Mhe.Muhagama ametoa takwimu ambazo
zinaonyesha kuwa Miradi ya Maendeleo iliyozinduliwa pamoja na kuwekewa
mawe ya msingi kupitia Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2015 ni miradi 1342
yenye thamani ya bilioni 463,519,966,467.
Pamoja na hayo amezitaja faida za
Mwenge wa Uhuru kuwa ni kuendelea kuamasisha ari ya wananchi kujitegemea
na kuwekeza katika maeneo mbalimbali katika Taifa letu,pia kimekuwa ni
chombo pekee cha kujenga umoja na mshikamano na kudumisha amani pale
unapopita bila kujihusisha na itikadi za kisiasa.
Aidha Mwenge wa Uhuru umeendelea
kuhamasisha na kuimarisha umuhimu wa Muungano kwa Watanzania wa pande
mbili za nchi yetu na kila mwaka huweka mawe ya msingi kwenye miradi
mbalimbali ya maendeleo ya wananchi na kuhamasisha uzalendo wa kuendelea
kujitolea.
No comments:
Post a Comment