Kamanda Mstaafu Tibaigana
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Kamanda Mstaafu Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam kuanzia mwaka 2001 hadi 2008, Alfred Tibaigana amesema
kuwa maandamano ya aina yoyote ni haki ya mwananchi na yanaruhusiwa
kisheria lakini maandamano hayo lazima yafuate sheria na taratibu
zilizobainishwa katika Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kamanda Tibaigana alitoa kauli
hiyo hivi karibuni katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi
kwa njia ya simu akisisitiza kuwa kila jambo linalofanyika hapa duniani
ni lazima liongozwe kwa Sheria na Kanuni.
Ingawa sheria nyingi za nchi
mbalimbali duniani zinafanana lakini kila nchi imejiwekea sheria na
kanuni za kufuata katika kufanya jambo lolote au katika kutafuta suluhu
ya migogoro mbalimbali ikiwemo ya kisiasa, kidini, kijamii pamoja na ya
kiuchumi.
Tanzania ni nchi mojawapo
inayoongozwa kwa Sheria na Kanuni mbalimbali na ndio sababu hata katika
Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa nchi imeeleza wazi kuwa hakuna aliye
juu ya sheria wala hakuna anayeruhusiwa kuzivunja sheria hizo.
Anasema kuwa ili Taifa litengemae
ni lazima wananchi wafuate Sheria na Kanuni zilizowekwa kwa sababu
kutofuata sheria ni kosa kubwa.
Tibaigana anaongeza kuwa Sheria ni
msumeno, ni vema kila pande ikaheshimu sheria na kanuni hasa kwa
kutambua madaraka ya kila mmoja yanaanzia wapi na yanaishia wapi ili
kuzuia tatizo la muingiliano wa majukumu ambao unaweza kusababisha
uvunjifu wa sheria na kanuni zilizowekwa na nchi husika.
Aidha, Katiba ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania imeelezea kwa undani pamoja na kuweka sheria na
kanuni zinazohusu maandamano ya aina yoyote ,yawe ya kisiasa, kidini,
kijamii au ya kiuchumi.
“Sheria inamtaka mwananchi au
kundi la wananchi wanaohitaji kufanya maandamano kutoa taarifa kwa
maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa eneo husika kabla ya masaa 48 ya kuanza
kwa maandamano hayo ikieleza dhumuni la maandamano hayo, pia wahusika
wanatakiwa wawe tayari kwa jibu lolote kutoka kwa mkuu huyo kwa kuwa
chochote watakachojibiwa lazima kiwe na sababu”, anasema Tibaigana.
Tibaigana anafafanua kuwa kama
wahusika watakataliwa kufanya maandamano na hawatoridhishwa na sababu
zilizotolewa na Mkuu wa Polisi kuna hatua mbili muhimu zinazotakiwa
zifuatwe na sio wahusika kujiamulia kuandamana kilazima kwa kuwa kufanya
hivyo ni kosa.
Hatua hizo muhimu zinazotakiwa
kufuatwa ni kuandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na
kumueleza kuwa hawajaridhika na sababu zilizotolewa na Mkuu wa Polisi
ili waziri naye kwa upande wake aamue kuruhusu au kukataza, endapo
wahusika hawatoridhika na majibu ya waziri, watatakiwa kwenda Mahakamani
ambapo ndipo uamuzi wa mwisho utatolewa.
Anasisitiza kuwa hakuna sheria
inayotambua maandamano ya nchi nzima kufanyika kwa siku moja kwa sababu
kila eneo lina Mkuu wa Polisi mwenye haki ya kukubali au kukataa ombi la
kufanya maandamano kulingana na hali halisi ya eneo lake.
Kila jambo lina faida na hasara
zake lakini kuna mambo ambayo faida huwa chache kuliko hasara,
maandamano yana athari kubwa kiuchumi na kijamii kwa sababu maandamano
yoyote ni lazima Jeshi la Polisi liwajibike katika kuongoza na kulinda
maandamano hayo, hivyo kupelekea wanajeshi wengi kusitisha kazi zingine
kwa ajili ya kuzuia vurugu zisitokee.
Athari zingine ni kusitishwa kwa
shughuli mbalimbali zikiwemo za usafiri , kufungwa kwa maduka na masoko
pamoja na athari zitokanazo na vurugu zinazoweza kutokea kwa sababu ya
maandamano hayo.
Aidha, Kamanda Tibaigana anatoa
ushauri kwa vyama vya siasa vinavyotumia maandamano kama njia ya kupata
usuluhishi wa migogoro yao kufata sheria na kanuni zilizowekwa kwani
maandamano mengi ya aina hiyo yanasababishwa na kutaka nafasi ya
kuongoza nchi kwahiyo kama chama hakitoheshimu sheria za nchi lazima
kiwe mfano mbaya kwa wananchi watakaowaongoza.
Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa
maandamano sio njia pekee ya kusuluhisha migogoro yao bali njia bora ni
kukaa chini na kuelewana kwa njia ya mazungumzo, huo ndio utamaduni wa
nchi yetu kwani hali hiyo ya kutii sheria na kanuni umepelekea nchi
kuendelea kuwa na amani wakati wote.
“Sisi ndio walinzi wa amani hiyo kwahiyo yatupasa kuzitii sheria zetu ili kuitunza amani yetu daima”.
No comments:
Post a Comment