Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Maofisa Misitu wanne na kusimamisha shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu wilayani Rufiji kwa muda usiojulikana baada ya kutoridhishwa na usimamizi wake.
Maofisa waliosimamishwa kazi ni
pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Dk. Paul
Ligonja, Ofisa Misitu wilaya Gaudens Tarimo, Ofisa Misitu Yonas Nyambuya
na Ofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa wilaya Seleman Bulenga.
Waziri Mkuu amefanya uamuzi huo
leo (Jumatatu, Septemba 26, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa
wilaya ya Rufiji kwenye ukumbi wa halmashauri kabla ya kuzungumza na
wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye viwanya jumba la maendeleo
wilayani Rufiji.
Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza
Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo kukusanya magogo yoye yaliyoko msituni
na kuyapiga mnada na kuitaka wizara ya Maliasili na Utalii kwenda
wilayani Rufiji kufanya uchunguzi wa leseni za uvunaji walizozitoa kwa
wilaya hiyo.
Waziri Mkuu amebainisha kwamba
wilaya ya Rufiji ni moja kati ya wilaya inayoongoza kwa uvunaji wa mazao
ya misitu bila ya kufuata taratibu licha ya kuwa na maofisa misitu.
“Hakuna mafanikio katika sekta ya
misitu kwenye wilaya hii ya Rufiji. Nasimamisha shughuli zote za
uvunaji wa mazao ya misitu pamoja na watendaji wake kwa sababu hatuwezi
kuacha watu wanakata magogo bila ya kufuata taratibu,”
“Haiwezekani Rufiji iwe shamba la
bibi, nimesimamisha uvunaji wa magogo hata kwa wenye leseni hadi
tuzichunguze zimetoka wapi. Hatuwezi kuruhusu maofisa wanashiriki
vitendo vya hujuma kwa kuvuna misitu Rufiji na kugonga mihuli ya Kilwa
kisha fedha wanatia mifukoni,” amesema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Rashid Salum
kufuatilia maagizo aliyoyatoa kuhusu kizuizi cha Ikwiriri kwa Waziri wa
Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alipokutana na watumishi wa
wizara hiyo.
Julai 18 mwaka huu Waziri Mkuu
alikutana na watumishi wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam na
kusisitiza kwamba hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi
wasiokuwa na uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.
Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo
kupunguza idadi ya vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya misitu kwenye
barababara mbalimbali baada ya kukosa tija, alitoa mfano wa barabara
ya kwenda mikoa ya kusini kuanzia Dar es Salaam yenye vizuizi
visivyopungua sita na kila kizuizi kinatumika kwa ajili ya kukagua mazao
ya misitu na maliasili inayotoka kuvunwa.
Awali mbunge wa Rufiji Mohammed Mchengelwa alilalamikia
vitendo vya dharau vinavyofanywa na watumishi wa sekta mbalimbali katika
wilaya hiyo jambo linalosababisha wananchi kukosa imani na Serikali
yao.
No comments:
Post a Comment