Friday, 30 September 2016

Mahakama yabariki urais wa Nkurunziza

 Image result for pierre nkurunziza
Uamuzi huo ulitolewa  na Mahakama ya Katiba ya Afika Mashariki (EACJ) kutokana na kesi iliyofunguliwa dhidi yake na asasi tatu za kiraia za Burundi, ambazo zilidai amejiongezea muda wa uongozi kinyume cha katiba.
Kupingwa kwa Rais Nkurunziza kuendelea kuwa rais kwa awamu tatu, kulisababisha kuibuka jaribio la kumpindua Mei, mwaka jana, chini ya Meja Jenerali Godefroid Niyombane.
Kutokana na kuongoza jaribio hilo, Meja Jenerali Niyombane alitimuliwa ukuu wa usalama, ikiwa miezi mitatu baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Mapema nchini humo, Mahakama ya Katiba ilimthibitisha Nkurunziza baada ya uteuzi wa chama chake cha CNDD FDD kumpitisha kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu.
Hukumuiliyosomwa jana na Jaji Isack Lenaola, ilithibitisha uhalali wa Rais Nkurunziza kuendelea kuongoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu kwa mujibu wa Katiba.


Jaji Lenaola alisema walalamikaji hao, ambao ni Jukwaa la Asasi za Vyama vya Kiraia katika nchi za Afrika Mashariki (EACSOF), Chama cha Wanasheria wa Afrika (PALU) na Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) hawakukidhi kigezo cha kisheria kufungua kesi na kwamba ilifunguliwa nje ya wakati.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa Katibu Mkuu wa EAC, Tume ya Uchaguzi ya Burundi (CENI) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Burundi. Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi iliondolewa katika orodha kutokana na kutokuwa na sifa ya kushtakiwa katika mahakama hiyo.

Walalamikaji waliitaka mahakama hiyo kutengua uamuzi wa Mahakama ya Katiba ya Burundi, uliothibitisha jina la Rais Pierre Nkurunziza kuwa mgombea urais aliyeteuliwa na chama chake.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Lenaola alisema mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kutafsiri hukumu iliyotolewa na
Mahakama ya Katiba ya Burundi na kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa nchi husika.

Hata hivyo, Wakili wa Chama cha Wanasheria wa Afrika (PALU), Evelyn Chijorira, alisema hajaridhishwa na hukumu hiyo na wanatafakari kukata rufani.

Mwanasheria wa Serikali ya Burundi, Nestory Kayobera, akizunguma baada ya hukumu hiyo, alisema mahakama imetenda haki kwa kuzingatia hukumu ya awali na sheria za nchi hiyo.

‘Maombi ya walalamikaji hayakuwa na msingi wowote wa kisheria bali yalisukumwa na hisia binafsi bila kuzingatia utashi na maslahi mapana ya wananchi wa Burundi,” alisema.

No comments:

Post a Comment