Fatma Makame/ MCC
Wananchi wa kijiji cha Chaani
Wilaya ya Kaskazin ‘A’ Unguja wamelalamikia ubovu wa barabara
inayoelekea Mkwajuni ambayo imekuwa kero kubwa kwao na wananchi wengine
wanaotumia barabara hiyo.
Akizungumza na Mwandishi wa
habari hizi Bi. Neema Mchezo Bakari amesema tatizo hilo ni la muda
mrefu na bado halijapatiwa ufumbuzi jambo ambalo linapelekea usumbufu
katika harakati zao za kutafuta maendeleo.
Amesema wananchi wanapata
usumbufu mkubwa kutokana na kuwepo mashimo katika barabara hiyo na
kupelekea baadhi ya madereva kukataa kupita na wengine kuendesha gari
kwa kasi bila kujali mashimo hayo na kusababisha ajali.
“Inafika wakati wajawazito
kujifugulia njiani kwenye gari wakati wanapopelekwa hospitali kutokana
maumivu wanayoyapata kutokana na mashimo yaliyomo katika barabara
hiyo”, amefahamisha mwananchi huyo.
Nae Chum Juma Simai amesema
ubovu wa barabara hiyo umechangia baadhi ya madereva wa gari za abiria
kutoza nauli kubwa kinyume na taratibu zilizowekwa na serikali na
kuitaka mamlaka husika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Nae Mkandarasi Mkuu wa Idara ya
Ujenzi na Utunzaji wa Barabara Nd. Jafeti amesema serikali tayari
inalishughulikia tatizo la barabara hiyo na ujenzi utaanza baada ya
kukamilika hatua za kumpata mkadarasi na kuwataka wananchi kujenga
subira na ustahamilivu.
No comments:
Post a Comment