Mkuu wa Kituo cha polisi Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP Evarest Makala akizungumza juzi
na wamiliki na madereva wa pikipiki katika warsha iliyoandaliwa na
mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
Mmiliki wa pikipiki Abubakary Sadiq
akizungumza juzi mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Mnayara
kwenye warsha iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi
kavu na majini (Sumatra).
Wamiliki na madereva wa pikipiki za
kubeba abiria (bodaboda) wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro
Mkoani manyara, wakiwa katika warsha iliyoandaliwa juzi na mamlaka ya
udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani
Manyara, Mhandisi Zephania Chaula amewataka wamiliki na madereva wa
pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) kujiandaa kulipia mapato kupitia
leseni ya usafirishaji wa abiria.
Mhandisi Chaula aliyasema hayo mji
mdogo wa Mirerani, akizungumza na wamiliki na madereva wa pikipiki za
kubebea abiria (bodaboda) kwenye semina iliyoandaliwa na mamlaka ya
udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
Alisema wanapaswa kujiandaa na
ulipaji wa leseni ya usafirishaji itakayoanza kutozwa hivi karibuni
kwani haikwepeki, hivyo wajipange kwa ajili hiyo ili wachangie mapato ya
nchi, ambayo inalenga kujitegemea.
“Hivi karibuni tutawapa taarifa ya
kuanza kwa zoezi hilo ila sasa subirini kidogo kwani hii ni serikali ya
awamu ya tano inayotaka kujitegemea kupitia mapato ya wananchi na siyo
kuomba misaada nje ya nchi,” alisema Mhandisi Chaula.
Afisa mfawidhi wa Sumatra mkoani
Manyara, Nelson Mmari alisema lengo la kukutana na bodaboda hao ni
kuhakikisha kila mmiliki anakuwa na leseni ya usafirishaji inayotolewa
kupitia halmashauri ya wilaya husika.
Mmari alisema Machi 2009, Bunge
lilipitisha sheria ya kuruhusu pikipiki za magurudumu mawili au mitatu
kubeba abiria kwa malipo au kukodisha na iliyoanza kutumika mwaka 2010
hivyo leseni ya usafirishaji inapaswa kulipiwa.
Alisema kila mtu anapaswa awe na
leseni ya usafirishaji wa biashara ya kubeba abiria wa pikipiki ya
magurudumu mawili au matatu na atakayekiuka atatozwa faini ya kati ya
sh50,000 au sh100,000 au kufungwa jela miezi sita au mwaka.
Alisema mkuu wa wilaya ya Simanjiro
aliwaelewesha vizuri wamiliki na madereva wa bodaboda kuwa wajiandae na
zoezi la ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwani zoezi hilo linatarajia
kuanza hivi karibuni kwenye eneo hilo.
Kwa upande wake, mkuu wa askari
polisi wa usalama barabarani wa mkoa wa Manyara, Mary Kipesha, alisema
wanasubiri taarifa ya mkuu wa wilaya hiyo ili waanze zoezi la
ufuatiliaji ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwa bodaboda.
“Tunasubiri mazungumzo hayo ila
mjiandae na ninyi kwani baada ya hapo ndipo tutaanza ukamataji kwa wale
ambao watakuwa hawajalipa leseni ya biashara ya kubeba abiria kwa wenye
bodaboda hapa Mirerani,” alisema Kipesha.
No comments:
Post a Comment