Thursday, 29 September 2016

Serikali yatenga Bilioni100 ukarabati wa viwanja vya ndege

irin
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli imetenga kiasi cha sh. Bil. 100 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini.
Rais Dk. Magufuli alisema hayo juzi katika sherehe za uzinduzi wa ndege mbili za Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na serikali, kwenye Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo viwanja hivyo vitaboreshwa ili kuwezesha ndege hizo kutua bila wasiwasi.
Mhe. Rais akifafanua zaidi, alisema , kiwanja cha ndege cha Nduli kilichopo umbali wa kilometa 13 Kaskazini Mashariki mwa Manispaa ya Iringa, ambacho kipo kwenye kiwango cha lami kitakarabatiwa, ili ndege hizo zitue na kupaa bila tatizo.
Dk. Magufuli alisema, kiwanja cha Nduli Iringa ni kiunganishi kikubwa na JNIA na kitatumika kupeleka watalii wanaokwenda kutembelea mbuga ya wanyama ya Ruaha, wakitokea Mataifa mbalimbali duniani.
Alisema mbali na kiwanja hicho cha Nduli, pia kiwanja cha Musoma kitawekwa lami, ili nacho kiwe moja ya maeneo ndege hiyo itakwenda, na kurahisisha usafiri wa watalii watakaokwenda kwenye mbuga ya wanyama ya Serengeti. Kwa sasa kiwanja cha Musoma kipo katika kiwango cha changarawe na kinatumika kwa ndege mbalimbali kutua na kupaa.
Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Nduli, Bi. Hannah Kibopile, kiwanja hicho kinapokea ndege ndogo zaidi ya saba zenye uwezo wa kubeba abiria 13, na kati ya hizo tatu zipo kwenye ratiba maalum ya kila siku na zilizosalia ni za kukodishwa na nyingine zinakwenda mbuga ya wanyama ya Ruaha.
Bi. Kibopile alisema ndege zinazotua kwenye kiwanja hicho zinatoka Jijini Dar es Salaam, Sumbawanga, Songea na Mbuga ya Ruaha.
Naye Kaimu Meneja wa Musoma, Bi. Faraja Mayugwa amesema kiwanja hicho kinapokea ndege zaidi ya nne kwa siku na nyingi zinakuwa za kukodi zinazopeleka watalii mbugani.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema “Hii ndege inaweza kutua katika kiwanja cha aina yeyote; na serikali itaendelea na ukarabati wa viwanja vya ndege vya pembezoni, ili viwe katika kiwango, ambacho ndege hizi zitatua na kuruka bila wasiwasi,”.
Akifafanua zaidi Dk. Magufuli alisema serikali inatarajia kununua ndege nyingine kubwa mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 160 na 242, ambazo zitaanzia safari zake kwenye JNIA kwenda sehemu mbalimbali duniani kama China au Marekani moja kwa moja, ikiwa ni lengo la kupata abiria hao, ambao wengi wao watakuwa watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali. Bombardier inauwezo wa kubeba abiria 76.
Naye Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof Makame Mbarawa awali wakati akimkaribisha Mhe. Rais kuzungumza na wananchi katika ghafla hiyo ya uzinduzi wa ndege, alisema kwa kuanzia ndege hizo zitatua kwenye viwanja 11 vya ndege, ambavyo ni Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro (KIA), Zanzibar (AAKIA), Mwanza, Dodoma, Arusha, Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya na  Mtwara.  Pia ndege hiyo itakwenda Comoro.
Mhe. Prof. Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa kuangalia viwanja  vingine vya ndege, ambavyo ndege hizi zitakwenda.

No comments:

Post a Comment