Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam
WAZIRI wa Mambo ya ndani ya nchi
Mwigulu Nchemba anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Mwaka
wa 47 wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya utakaofanyika kuanzia
Septemba 30 hadi Octoba 2 mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa
Jumuiya hiyo Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, Katibu Mkuu Msaidizi
Abdurahman Ame alisema kuwa mkutano huo utafanyika eneo la kitonga, kata
ya Msongola Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Alisema Jumuiya imeandaa mkutano
huo kwa lengo la kuhamasisha amani katika jamii na kuwakumbusha waumini
hasa wa kiislamu juu ya misingi sahihi ya dini ya kiislamu pamoja na
kumjua na kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu.
“Wajibu wa kiongozi wa dini ni
kuandaa na kuhamasisha masuala ya dini, hivyo lengo la mkutano huo ni
kuhamasisha amani katika jamii na pia kuwakumbusha waumini wa kiislamu
juu ya kumjua, kuishi na kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu hali
itakayosaidia kuondokana na vitendo viovu,” alifafanua Katibu huyo.
Mbali na hayo, mkutano huo
utabebwa na kaulimbiu isemayo “kuitambua amani ya jirani yako,
huvunjilia mbali kuta zinazowatenganisha” ikiwa na ujumbe ya kwamba kuna
haja ya kuelimisha jamii uzuri wa mafundisho ya dini kwa kutumia vitabu
vitakatifu kupitia vyombo mbalimbali vya masasiliano.
Vile vile, Washiriki mbalimbali
kutoka ndani na nje ya nchi zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Malawi,
Msumbiji na Uingereza wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za
kidini na za kijamii watashiriki katika mkutano huo.
Ahmadiyya ni jumuiya ya waislamu
ya kimataifa iliyoenea katika nchi 209 duniani kwa lengo la kuleta
uhuisho wa dini ya kiislamu kwa kutangaza kwa amani ujumbe sahihi wa
Islam duniani kote.
No comments:
Post a Comment