Wananchi 365 wa kijiji cha
Chongoleani watafidiwa shilingi bilioni 3,035 kwa ajili ya kutoa maeneo
yao, ili kupisha ujenzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Hoima
nchini Uganda mpaka Tanga.
Hayo yamesemwa na Meneja
Mawasiliano wa Shirika la Usimamizi wa Bandari Tanzania TPATanga, Bibi
Janeth Rwuzangi katika mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO)
leo.
Bi Ruzangi amesema kuwa kwa
hapa Chongoleani mradi una ukubwa wa hekta 200 zikiwemo hekta 100
zitakazotumiwa kuweka miundombinu ya mafuta ghafi. Hekta 100 zilizosalia
zitatumika kwa ajili ya shughuli za TPA) kuwekeza miundombinu ya
kupokea mafuta yaliyosafishwa. Vile vile eneo hili limezingatia
maendeleo endelevu ya biashara ya mafuta na gesi katika siku zijazo.
Aliongeza kuwa TPA itakuwa na
wajibu wa kuhudumia meli, kuhakikisha usalama wa bidhaa, vyombo na watu
pamoja na kusimamia masuala ya afya bandarini. Aidha, Majukumu la TPA
yanatarijiwakujikita katika shughuli za uendeshaji wa majini ikiwemo
kuwa na vyombo na boti maalumu kwa ajili ya kuongozea meli wakati wa
kuingia na kutoka kwenye gati la mafuta ghafi.
Akitoa ufafanuzi, Bi Ruzangi
amesema vile vile, TPA ina jukumu la kuhakikisha inahudumia shehena ya
vifaa vyote vya ujenzi katika Bandari ya Tanga kwa kushirikiana na
Bandari Kuu ya Dar es Salaam. Shughuli nyingine ni pamoja na ulinzi wa
miundombinu ya majini pamoja na usalama wa eneo la Bandari ambalo
limegawanyika katika sehemu kuu mbili; ardhini kwenye gati la mafuta na
majini kwenye lango la kuingilia meli na nangani.
Kwa upande wa ajira za TPA
Ruzangi amesemawafanyakazi ambao wataajiriwa ni pamoja na mabaharia,
wahandisi, mafundi, wahasibu, wachumi, watakwimu, vibarua mbalimbali kwa
ajili ya nguvu kazi n.k. Sehemu ya wafanyakazi hawa watatokana na
waliopo sasa kwenye Bandari watakaopangiwa kazi hizo. Hata hivyo TPA
inatarajia kuajiri wengine ambao watalazimika kufanya kazi hizo
kulingana na taratibu za ajira za TPA.
Pamoja na kuwa na bomba la
mafuta, kijiji cha Chongoleani kitafaidika na ujenzi wa barabara ya
kilometa 8 itakayounganisha bandari na barabara kuu ya Horohoro – Tanga,
ambapo kwa kiasi kikubwa itainua uchumi wa wananchi wanaoishi maeneo
hayo kusafirisha mazao, samaki na bidhaa nyingine kwa urahisi.
Akifafanua uwekaji wa jiwe la
msingi Ruzangi amesemakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt,
John Pombe Magufuli na Mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni
wanatarajia kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta tarehe 05
Agosti 2017.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha
Chongoleani, Bw. Mbwana Nondo amesema; “Kwa moyo wa dhati kabisa, naomba
nimshukuru sana sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John
Pombe Magufuli kwa kutujali wananchi wake na kutuletea neema ya Mradi wa
Bomba la Mafuta, katika maisha yetu wanachongoleani, hatutaweza
kumsahau kwa kizazi hiki kinachoshuhudia mradi huu na vizazi vijavyo”.
Nondo alisema kuwa anamuhakikishia
Mhe. Rais kuwa kuwa wote watakaopata fursa kwenye mradi wa Bomba la
Mafuta, watafanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja
mmoja na Taifa kwa ujumla.
Bomba la Mafuta la kutoka Hoima
Uganda mpaka Tanga Chongoleani lina urefu wa Kilometa 1445 ambapo kwa
upande wa Tanzania itakuwa na jumla ya kilometa 1115 na Uganda 330.
Aidha, Mradi utatarajia kusafirisha mapipa laki mbili na kumi na sita
elfu (216,000) kwa siku .
Kijiji cha Chongoleani ndio
kituo cha mwisho ambapo mitambo mikubwa itasimikwa katika eneo hili kwa
ajili ya kusukuma mafuta eneo la baharini ili, kuweka kwenye vyombo vya
usafirishaji kusafirisha maeneo mbalimbali duniani ambayo Uganda
watakuwa wamepata soko.
Tanzania itafaidika na mradi
huu kutokana na kodi, tozo na mrahaba wa bomba la mafuta, itakayofanywa
moja kwa moja na mradi huo. Faida nyingine ambazo, sio za moja kwa moja
ni ajira, fursa za kufanya biashara na uwezekano wa mikoa 8 ambayo ni
Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro na Tanga.
No comments:
Post a Comment