Tuesday, 22 August 2017

Marekani yataka uchunguzi kuhusu ajali ya meli yake ya kivita

Jeshi la wanamaji la Marekani limeagiza uchunguzi kufanyika katika kundi lake la meli za kivita katika Bahari ya Pacific baada ya meli yake moja ya kivita kugongana na meli ya kubeba mafuta karibu na Singapore.
Uchunguzi huo utaangazia "ajali zote zinazohusiana (na ajali hiyo) ambazo zimetokea baharini," Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis amesema akiwa Amman, Jordan.
Mabaharia kumi wa jeshi la wanamaji la Marekani bado hawajulikani walipo baada ya ajali hiyo iliyotokea mapema Jumatatu asubuhi.
Afisa mkuu wa jeshi la wanamaji John Richardson, mkuu wa shughuli la jeshi hilo, amemwamuru Phil Davidson, mkuu wa makundi ya meli za jeshi hilo baharini kuongoza uchunguzi huo.
Jenerali Mattis amewaambia wanahabari Jumatatu kwamba uchunguzi huo pia utaangazia ajali ya Juni ambapo meli ya kivita ya USS Fitzgerald iligongana na meli ya kubeba mizigo katika eneo la bahari la Japan, ambapo mabaharia saba walifariki.
Bw Richardson amesema anataka kuhakikisha kwamba hakuna matatizo mengine makubwa katika meli zinazohudumu bahari ya Pacific, shirika la habari la AP limesema, likimnukuu afisa wa wizara ya ulinzi wa Marekani.
Meli ya USS John S McCain yenye uwezo wa kurusha makombora ilikuwa baharini mashariki mwa Singapore na ilikuwa ikijiandaa kutia nanga bandarini pale ilipogongana na meli ya kubeba mafuta iliyokuwa inapeperusha bendera ya Liberia.


Tunafahamu nini kuhusu ajali hiyo?
Ajali hiyo iliripotiwa mwendo wa saa 05:24 saa za huko Jumatatu (21:24 GMT Jumapili) na ilitokea mashariki mwa Mlango wa Bahari wa Singapore, ambapo USS John S McCain ilikuwa inajiandaa kuingia bandarini kama kawaida Singapore.
Maafisa wa Singapore na Marekani wamesema meli hiyo iliharibiwa upande wake wa kuingia kilindini, ambao ni upande wa kushoto wa meli hiyo ukiangalia mbele.


Meli ambayo iligongana na manowari hiyo, Alnic MC, iliharibika tangi lililo karibu na sehemu ya mbele ya meli hiyo, mita saba (23ft) juu ya maji ya bahari, lakini hakuna baharia aliyejeruhiwa wala hakuna mafuta yaliyomwagika.

Meli hiyo yenye urefu wa 182m (600ft), ni ndefu kidogo kuliko manowari hiyo ya Marekani yenye urefu wa 154m.

Kunatokea nini sasa?
Helikopta za jeshi la Marekani zikishirikiana na majeshi ya wanamaji wa Singapore na Malaysia wanafanya juhudi za uokoaji kuwasaka mahabaria waliotoweka.

Maswali chungu nzima

Ajali hiyo imetokea Marekani ikiendelea kufanya mazoezi ya kila mwaka kati ya majeshi yake na Korea Kusini, kuonyesha ubabe dhidi ya Korea Kaskazini.

USS John McCain ni sehemu ya kundi la meli za 7th Fleet, kundi kubwa zaidi la meli za kivita za Marekani, na ajali hiyo itaibua maswali kuhusu shughuli za jeshi la wanamaji la Marekani eneo hilo.

Meli ya USS Fitzgerald ilikuwa ya kundi hilo pia. Wiki iliyopita, Marekani ilisema mabaharia kadha waliohusika wangeadhibiwa.

Hii inaaminika kuwa ajali ya nne ya aina hiyo iliyohusisha meli za kivita za Marekani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Ukiongeza suitafahamu iliyokuwepo kuhusu meli ya kubeba ndege za kivita ya USS Carl Vinson mapema, Trump aliposema ilikwua inaelekea upande wa Korea Kaskazini, lakini ikawa inaelekea upande kinyume, kunazua maswali zaidi.

No comments:

Post a Comment