Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limevitaka baadhi ya vyombo vya habari nchini kuacha mara
moja kampeni za upotoshaji zenye lengo la kuwachafua viongozi wa juu wa
shirikisho hilo.
TFF imeshtushwa na taarifa
inayoendelea kutolewa kwenye gazeti moja la kila siku ikidai kuwa kuna
ufisadi ndani ya shirikisho wakati madai hayo ni ya uongo na yenye lengo
la kujenga mtazamo hasi dhidi ya shirikisho na viongozi wake.
Gazeti hilo la kila siku limetumia
taarifa ya ukaguzi wa fedha iliyofanywa na wakaguzi kutoka TAC kujenga
picha kuwa ni ushahidi tosha wa kuwepo kwa ufisadi ndani ya shirikisho.
Taarifa ya ukaguzi wa fedha ya TAC
haikuwahi kuituhumu TFF kwa ufisadi. Taarifa ilibaini maeneo ya
kiuhasibu ambayo yalihitaji maelezo ya ziada ya namna baadhi ya malipo
yalivyofanyika (audit queries), na ufafanuzi ulitolewa kwa ufasaha na
watendaji wa shirikisho na kupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu wa
Shirikisho.
Hata hivyo gazeti hilo ambalo
limeonekana kuweka kando kabisa misingi ya uandishi wa habari,
limechapisha taarifa bila hata kutoa nafasi kwa wanaotuhumiwa kujibu na
kutoa ufafanuzi stahiki.
Rais na katibu mkuu wa shirikisho
wanahudhuria mikutano ya CAF nje ya nchi wakati gazeti hilo likiendelea
kuporomosha mlolongo wa tuhuma bila kutoa haki ya kusikilizwa kwa
wanaoandikwa vibaya.
TFF inaliangalia suala hili kama
kampeini chafu inayofanywa ili kushawishi matokeo ya uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika mwezi Agasti mwaka huu.
Pia taarifa hii potofu inalenga
kulihamisha taifa kutoka kwenye masuala ya msingi kama kuiunga mkono
Serengeti Boys kwenye mashindano ya Afrika na kuanza kujadili masuala
yanayohusiana na siasa za uchaguzi wa TFF.
TFF kwa sasa inatafakari hatua za
kisheria za kuchukua dhidi ya vyombo vya habari husika na inachukua
nafasi hii kuvisihi vyombo vya habari kuacha mara moja kujihusisha na
kampeni ya kuchafuana ambayo ni kinyume na misingi ya maadili ya
uandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment