Kamishna wa Madini Tanzania
Mhandisi Benjamini Mchwampaka akizungumza jambo wakati wa Kufunga
Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito ya Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho
Gambo (katikati), Waziri wa Madini na Maendeleo ya Viwanda wa Nigeria
Abubakar Bwari (wa pili kulia), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na
Maendeleo ya Viwanda wa Nigeria, Abbas Mohamed (wa kwanza kulia) ,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Arusha Peter Pereira ( wa kwanza
kushoto ) na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania
Sam Mollel (wa pili kushoto) wakifuatilia kutangazwa kwa washindi wa
Mnada wa Madini ya Tanzanite.
Kamishna wa Madini Tanzania
Mhandisi Benjamin Mchwampaka (katikati) akikata kamba maalum katika
masunduku yaliyowekwa bahasha za walioomba kununua madini ya Tanzanite
kupitia mnada. Kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la
Taifa, (STAMICO) Mhandisi Hamis Komba na kushoto ni Mwakilishi kutoka
Kampuni ya TanzaniteOne, Husein Gonga.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho
Gambo (kulia) akiangalia zawadi kabla ya kumkabidhi Waziri wa Madini na
Maendeleo ya Viwanda wa Nigeria, Abubakar Bwari (kushoto).
Waziri wa Madini na Maendeleo ya
Viwanda wa Nigeria, Abubakar Bwari (katikati) akiangalia ubora wa Madini
ya Tanzanite katika banda la kampuni ya Hadjarat Mining and Gemstone
Company Limited. ALiyeshika kifaa cha kupima ubora ni Mkurugrenzi wa
Kampuni hiyo.
Baadhi wa washiriki wa Maonesho
ya 6 ya Madini ya Vito Arusha wakiwemo wanunuzi na wauzaji wakifuatilia
hatua za kumpata mshindi wa Mnada wa Madini ya Tanzanite.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya SDK
Limited, Susie Kennedy akimwonesha Waziri wa Madini na Maendeleo ya
Viwanda wa Nigeria, Abubakar Bwari bidhaa za madini zinazotengenezwa na
kampuni hiyo.
Na Asteria Muhozya, Arusha
Wadau wa Madini nchini wametakiwa
kujikita katika shughuli za ukataji na usanifu wa madini badala ya
kusanifiwa nje ya nchi ili kuwezesha adhma ya Serikali ya Tanzania ya
Viwanda kupitia Sekta ya Madini.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa
Madini Tanzania, Mhandisi Benjamini Mchwampaka wakati wa kufunga
Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha
kuanzia tarehe 3-5 Mei,2017.
Aliongeza kuwa, uwepo wa shughuli
za ukataji na unga’rishaji wa madini hayo nchini kutawezesha
kuyaongezea thamani ikiwemo kupanua wigo wa ajira kupitia sekta ya
madini.
” Tanzania ya sasa ni ya Viwanda.
Na sisi sekta ya madini tuwe na viwanda vyetu vya kusanifu madini yetu
hapa hapa nchini. Kwanza tutayaongezea thamani madini yetu lakini pia
tutazalisha ajira kwa wingi,” alisema Mchampaka.
Aidha, Kamishna Mchwampaka
aliongeza kuwa, tayari Wizara ya Nishati na Madini imewasiliana na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri
ya biashara ya Madini nchini ili kuondoa kero ambazo ni kikwazo
katika biashara hiyo kwa watanzania.
“Tunataka kuweka mazingira mazuri
zaidi kwa wafanyabiashara wa madini wa Tanzania lakini pia tunapenda
wafanyabiashara wetu washiriki kwa wingi katika maonesho haya. Ni fursa
kubwa ya kibiashara kwao,” alisisitiza Mchwampaka.
Akizungumzia Mnada wa Madini ya
Tanzanite uliofanyika tarehe 5 , Mei, alisema kuwa, minada hiyo
itaendelea kufanywa mara kwa mara kutokana na mchango wake katika sekta
husika kwa kuwa pia inasaidia kupata bei halisi ya madini hayo.
Katika mnada wa Madini ya
Tanzanite jumla ya kampuni 48 zilishiriki mnada huo ambapo madini ghafi
ya Tanzanite kutoka Kampuni ya TanzaniteOne yenye jumla ya gramu
691,060.33 ziliuzwa katika mnada huo kwa dola za Marekani 3,161,860,
sawa na asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa kwa mauzo.
Pia, alizungumzia ujumbe wa
Serikali ya Nigeria iliyoshiriki Maonesho hayo na kueleza kuwa, ujumbe
huo ulifika kwa lengo la kujifunza namna Tanzania inavyoongeza thamani
madini yake ikiwemo pia kubadilisha uzoefu na kuongeza kuwa, lengo ni
kuifanya Afrika inufaike na rasilimali zake za madini.
Ujumbe wa Serikali ya Nigeria
uliongozwa na Waziri wa Madini na Maendeleo ya Viwanda, Abubakar Bwari
aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Abbas Mohamed pamoja na
ujumbe wa wafanyabiashara wa Madini kutoka nchini humo.
No comments:
Post a Comment