Monday, 5 September 2016

Serikali imeanza kutekeleza Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu

wat
Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Kamana Stanley (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kutekelezwa kwa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 inayolenga kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo Sheiba Bullu.
Picha/Fatma Salum –MAELEZO.

Na. Fatma Salum – MAELEZO.
 Dar es salaam.
Serikali imeanza kutekeleza Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 (The Whistleblower and Witness Protection Act. 2016) ili kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Kamana Stanley wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kutumika kwa sheria hiyo.
Stanley amesema kuwa  kuwepo kwa sheria hiyo kutasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa ya aina mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka. Vilevile itarahisisha utoaji na upatikanaji wa taarifa za uhalifu kwani sasa taarifa hizo zitatolewa na kupokelewa sio tu kwenye vyombo vya dola pekee bali pia kupitia vyombo vya habari na vyanzo vingine vinavyobainishwa katika sheria hiyo.
“Wananchi wasiwe na woga kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu na matendo ya aina zote yanayofanywa kinyume cha sheria kwani taarifa hizo zitakuwa siri na zitafanyiwa kazi bila ya kuwataja watoa taarifa. Pia mashahidi wanapotakiwa kufika mahakamani wasiogope kwani sheria hii inawalinda” amesema Stanley.
Amefafanua kuwa wahusika watakaoshindwa kushughulikia vyema taarifa zinazotolewa kwao na kuruhusu watoa taarifa na mashahidi kupata madhara, sheria hiyo imeweka utaratibu wa namna ya kushughulika nao.
Aidha, Stanley ameeleza kuwa katika sheria hiyo wale ambao taarifa zao zitafanikisha kuokoa mali ya umma, kupatikana kwa wahalifu na kulinda mazingira na maisha ya binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika, wamewekewa utaratibu wa kupatiwa motisha ikiwa ni pamoja na kuwafidia wale ambao wataathirika kutokana na taarifa walizotoa.
Stanley ameongeza kuwa Serikali inatarajia kwamba kutungwa kwa sheria hii kutaleta matokeo chanya katika kupambana na uhalifu wa aina zote hivyo kukuza ari ya wananchi kusimamia wenyewe juhudi za kujiletea maendeleo.
 
“Masuala ya usimamizi wa utawala wa sheria yataimarika kutokana na kuwepo kwa utayari wa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kufika katika vyombo vya sheria kutoa ushahidi. Pia ushiriki wao katika kufichua maovu yakiwemo yanayosababisha hasara kwa taifa utasaidia kuinua uchumi ukizingatia kwamba sasahivi Serikali inapambana sana na mafisadi” ameeleza Stanley.
Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 (The Whistleblower and Witness Protection Act. 2016)imeanza rasmi kutumika Julai Mosi mwaka huu baada ya kuidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe.

No comments:

Post a Comment